Israel yashambulia Gaza na kusababisha maafa
20 Machi 2025Wakati idadi ya vifo ikikaribia kufikia watu 1,000 ndani ya siku tatu za mashambulizi huko Gaza, Israel imesema usiku wa jana kuwa wanajeshi wake wamechukua tena udhibiti wa sehemu ya ukanda wa Netzarim unaoitenganisha Gaza sehemu mbili za kaskazini na kusini, huku Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz akionya kwamba mashambulizi yataongezeka hadi Hamas iwaachie makumi ya mateka na kujiondoa kabisa eneo hilo.
Jeshi la Israel liliondoka katika ukanda wa Netzarim mwezi Januari kama sehemu ya awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano ambayo sasa imefikia tamati huku mazungumzo ya kuurefusha mpango huo au kuingia awamu ya pili yakionekana kukwama. Usitishaji huo wa mapigano uliwapa ahueni japo kwa wakati mfupi Wapalestina waliochoshwa na vita vya zaidi ya miezi 15 na kuruhusu usambazaji zaidi wa misaada ya kibinadamu inayohitajika mno huko Gaza . Wapalestina wametaja kuchoshwa na hali hiyo kama anavyoeleza mmoja wao Nour Bakir:
"Hali hii itaendelea hadi lini? Sisi ni wagonjwa na tumechoshwa nayo. Wanasema sisi ni wastahimilivu? Sisi si wastahimilivu, bali tunakufa katika dunia hii. Waache watuangamize tupumzike madhila haya, tumechoka. Haya yataendelea hadi lini? Ninawaambia Wayahudi na Israel yote kwamba tunataka amani na watu wetu wote wanataka amani."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa kufuatia shambulizi la Israel kwenye jengo moja huko Gaza na kutaka ufanyike uchunguzi kamili. Israel imekana kuhusika na shambulizi hilo ambalo limewajeruhi pia wafanyakazi wengine watano wa Umoja wa Mataifa lakini ikasema itachunguza kwa makini tukio hilo.
Msemaji wa Guterres Farhan Haq amesema shambulio hilo huko Deir el-Balah limepelekea idadi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliouawa huko Gaza tangu Oktoba 7 mwaka 2023, kufikia 280. Hayo yanajiri wakati Israel imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi huko Gaza baada ya kukwama kwa mazungumzo ya amani.
Maelfu waandamana Israel kumpinga Netanyahu
Kuanza tena kwa mashambulizi ya anga kumezusha wasiwasi mkubwa huko Israel kuhusu hatima ya karibu mateka 20 wanaoshikiliwa na Hamas na ambao inaaminika kuwa bado wapo hai. Msemaji wa Hamas, Abdel-Latif al-Qanou, amesema hatua za hivi karibuni ni ishara tosha kwamba Israel imejiondoa moja kwa moja kwenye mchakato wa amani na imeanzisha tena mzingiro wake huko Gaza.
Maelfu ya raia wa Israel walimiminika mitaani jana kupinga sera na hatua za waziri mkuu Benjamin Netanyahu wakisema anadhamiria kuidhoofisha demokrasia huku wakimtaka ajiuzulu na kumtaja kama mhusika mkuu aliyewezesha janga hili lililoanza na mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7 mwaka 2023.
Soma pia: Mashambulizi ya Israel yaua zaidi ya 400 Gaza
Katika hatua nyingine, hali si shwari nchini Yemen ambako mashambulizi makali ya Marekani yameendelea kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi katika mji mkuu Sanaa na eneo la kaskazini magharibi la Saada, huku rais Donald Trump akitoa onyo kali kwa waasi hao kuwa atawaangamiza na kuitaka Iran ambayo ndiyo mfadhili mkuu wa waHouthi kusitisha uungwaji wake mkono.
Hayo yakiarifiwa, Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amefanya ziara nchini Lebanon na ameitolea wito Israel kuheshimu makubaliano ya usitishwaji mapigano kati yake na kundi la Hezbollah huku akiitaka kuviondoa vikosi vyake nchini humo. Baerbock ameitoa kauli hiyo mjini Beirut baada ya kukutana kwa mazungumzo na rais wa Lebanon Joseph Aoun.
(Vyanzo: Mashirika)