Iran, Israel zaendelea kurushiana makombora, droni
19 Juni 2025Mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Iran, mbali na kuwauwa makamanda wa juu wa jeshi la Iran yamewauwa mamia ya watu wakati kwa upande wa Tel Aviv kukiripotiwa kuwa zaidi ya raia 20 wameuwawa.
Katika shambulio la karibuni zaidi kwa upande wa Israel, hospitali kubwa ya Beersheba Kusini mwa taifa hilo imeshambuliwa huku Iran ikisema kuwa, kusudio lake lilikuwa kuishambulia kambi ya jeshi na kituo cha intelijensia na si hospitali.
Soma zaidi: Hali bado ni tete wakati Israel na Iran zikishambuliana vikali
Huko Tehran, mapema Alhamisi jeshi la Israel limearifu kuwa limeshambulia moja ya miundombinu muhimu ya kimkakati karibu na mji wa Arak, muda mfupi baada ya tahadhari iliyotolewa na Israel ikiwataka wakaazi wa mji huo kuondoka.
Wakati hayo yakiendelea, Rais Donald Trump ameendeleza utata kuhusu ikiwa Marekani itaungana na Israel kuishambulia Iran. Katika kauli yake ya Jumatano Trump alisema huenda akajiunga na mashambulizi hayo au asifanye hivyo. Zaidi amesema Iran imeonesha nia ya mazungumzo lakini huenda imechelewa kuchukua hatua hiyo.
Iran yaionya Marekani isithubutu kuishambulia kijeshi
Kwa upande wake kiongozi wa juu zaidi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amehutubia kupitia televisheni ya taifa kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo ulipoanza. Khamenei ameapa kuwa ikiwa Marekani itahusika kijeshi kuishambulia, itapata madhara ambayo hayawezi kurekebishika. Amesisitiza kuwa Iran haitajisalimisha na ameyalaumu mataifa ya magharibi kwa kupotosha kuhusu madhumuni ya Iran ya mpango wake wa nyuklia.
Soma zaidi: Iran yakataa Kujisalimisha: Khamenei aionya Marekani
Zaidi Khamenei alisema, "Adhabu ambayo taifa la Iran na vikosi vyake vya kijeshi vimeitoa, vinaendelea kuitoa sasa na vinapanga kuendelea kuitoa kwa adui huyu muovu ni adhabu kali ambayo imemdhoofisha adui huyo. Ukweli kwamba marafiki zake wa Kimarekani wanaingilia kati na kuanza kutoa matamko unaonesha udhaifu na kushindwa kwao."
Juhudi za kidiplomasia za kujaribu kuutatua mzozo huu bado zinaendelea wakati mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wakijiandaa kwa mazungumzo ya nyuklia na Iran Ijumaa mjini Geneva. Hadi sasa Marekani haijaonesha dalili zozote za kuwa na mipango ya kujiunga na mazungumzo hayo.