MASHAMBULIO YA WANAMGAMBO-IRAQ:
22 Novemba 2003Matangazo
BAGHDAD: Maroketi yaliofichwa katika mkokoteni wa punda yamerushwa katika wizara ya mafuta ya Iraq na hoteli mbili zinazotumiwa na wageni kutoka nchi za magharibi.Kuta za hoteli ziitwazo "Palestine" na "Sheraton" zilitoboka.Kwa mujibu wa watumishi wa hoteli Mmarekani mmoja alijeruhiwa na wageni wengine walihamishwa.Magari megine mawili yanayokokotwa na punda yaliopakiwa maroketi,yalikutikana karibu na balozi za Italia na Uturuki.Jemadari mmoja wa Kimarekani amesema wapiganaji wa chini kwa chini wa Kiiraqi wanazidi kuvumbua njia mpya za kuhujumu.Mashambulio ya Ijumaa yametokea baada ya Marekani kudai kuwa mashambulio ya angani ya Marekani katika wiki iliyopita,yamepunguza idadi ya mashambulio ya ghafla dhidi ya vikosi vya Kimarekani kwa asilimia 70.Kwa upande mwingine Hungary imearifu kuwa mwanafunzi wa nchi hiyo aliekuwa akifanya kazi nchini Iraq kama msaidizi aliejitolea kwa huduma za kiutu kando ya wanajeshi wa Poland,alifariki baada ya kupigwa risasi na vikosi vya Kimarekani.Mwanafunzi huyo kwa mwendo mkubwa alikikaribia kituo cha ukaguzi,kilicho upande wa magharibi wa mji mkuu Baghdad.