Mashabiki, joto na siasa: Kombe la Dunia la Vilabu
23 Juni 2025Mechi zisizokuwa na mvuto na viti vitupu, lakini pia tamasha la kandanda lenye msisimko mbele ya mashabiki wanaoshangilia: Kombe la Dunia la Vilabu nchini Marekani mpaka sasa limekuwa kinyang'anyiro chenye sura nyingi.
Mashabiki wa Amerika Kusini wanashamiri
Mpaka sasa Kombe la Dunia la Vilabu limekuwa hafla kubwa kwa timu za Amerika Kusini na mashabiki wao. Mashabiki wengi wa Botafogo uwanjani walipiga magoti baada ya kipyenga cha mwisho kusherehekea ushindi wao wa 1 – 0 dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Paris Saint-Germain.
Mashabiki wa Boca Juniors, nao, hawakuwa na Bahati baada ya miamba hao wa Argentina kuzabwa 2 – 1 na Bayern Munich. Lakini uwanja wa Hard Rock mjini Miami ulikuwa na msisimko mwanzo hadi mwisho hasa wakati Boca waliposawazisha na kufanya mambo kuwa 1 – 1 kabla ya kichapo.
Soma pia: FIFA isitishe mchakato wa kuipatia kibali Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia
Jukumu la siasa
Kiwango ambacho michezo na siasa vimeingiliana kinaweza pia kushuhudiwa katika Kombe la Dunia la Vilabu. Mkutano wa waandishi habari uliofanywa na Rais wa Marekani Donald Trump katika ofisi ya Oval iliwaweka wachezaji wa Juventus katika hali ya kushangaza. Wakati wachezaji wa Juve walikuwa wamesimama nyuma ya rais, Trump alijibu maswali kuhusu vita kati ya Israel na Iran na jukumu la Marekani.
Mashabiki wa Bayern, wakati huo huo, waliipinga FIFA uwanjani kwa kuonesha bango kubwa linaloukosoa uongozi wa FIFA.
Hali ya hewa
Halijoto kali na mechi kuchezwa katika joto la saa za mchana vimekuwa na athari inayoonekana wazi kwenye mashindano hayo.
Wachezaji wa akiba wa Borussia Dortmund awali walibaki kwenye chumba chao cha kuvalia uwanjani katika ushindi wao wa 4 – 3 dhidi ya Mamelodi Sundowns, badala ya kukaa wkenye benchi chini ya juwa kali.
Lakini sio joto kali tu ambalo ndio tatizo: kumekuwepo na matukio ya kuvurugwa mechi kwa kipindi kirefu kutokana na hatari ya kutokea dhoruba.
Kipindi cha pili cha mechi ya Benfica dhidi ya Auckland City kilianza kwa kuchelewa kwa saa mbili kwa sababu ya mvua kubwa na dhoruba mjini Orlando. Mechi kati ya Sundowns na Ulsan HD ilicheleweshwa kwa zaidi ya saa moja.
Kipindi cha pili cha mechi kati ya Palmeiras na Al Ahly mjini New Jersey kilicheleweshwa kwa dakika 40 na Salzburg v Pachuca mjini Cincinnati kikacheleweshwa kwa dakika 90 kutokana na kitisho cha hali ya hewa.
dpa