Serikali ya Kenya yawaonya wanaosaka ajira ughaibuni
3 Machi 2025Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora imefichua kuwa kundi hilo limekwama mpakani na ni miongoni mwa zaidi ya raia 7,000 wa kigeni waliokombolewa na makundi yenye silaha lakini bado hawawezi kuvuka mpaka kuingia Thailand tangu Februari 12. Kundi la kwanza la waathiriwa 260, wakiwemo Wakenya 23, liliruhusiwa kuingia.
Peter Mwangi mwenye umri wa miaka 28 alikwenda Thailand kutoka Kenya baada ya rafiki yake kumuarifu kuhusu nafasi ya wakufunzi nchini humo. Alikuwa na matumaini ya kufanikiwa kwani alisomea ualimu kwenye chuo kikuu cha Nairobi. Alilipa shilingi za Kenya laki moja na nusu kwa ajili ya usafiri.
Alipofika Bangok alichukuliwa na wenyeji wake ambapo aliajiriwa kufanya kazi ya kuwalaghai raia wa Marekani na Afrika kuja kufanya kazi mbali mbali nchini Thailand chini ya uangalizi wa mabosi wa Kichina karibu na mpaka wa Thailand na Mynamar kwa kipindi cha miezi minne. Alihitajika kufanya kazi kwa saa 19 kwa siku bila ya mshahara. Alihitajika kupata faida ya dola 10,000 za Marekani kwa siku ndiyo aachiliwe huru.
Mwangi alisema “Sikuelewa kilichoendelea, vile nilikataa wakachukua simu yangu, wakatoa laini yangu ya Safaricom wakaiharibu. Tuko mataifa mengi, tuko zaidi ya watu 7000 hapa.”
Baadhi washindia wali mweupe tu
Yeye na wenzake waliponea baada ya serikali ya China kuzishinikiza serikali za Mynamar na Thailand kuzifunga kambi zilizoko kwenye mipaka ya mataifa hayo mawili. Anasema kuwa awali walikuwa wamefungiwa kwenye chumba kidogo huku wakitumia choo kimoja kwenye mazingira mabaya, huku wali mweupe tu ukiwa ndio chakula tu.
Soma pia:Ujerumani, Kenya kuimarisha Mafunzo ya Kijerumani na fursa za ajira
Sawa na raia wa Bangladesh, Ethiopia, Somalia na wengine wengi kutoka nchi nyingine waliokwama kwenye mpaka huu sasa Peter anaiomba serikali ya kenya imsaidie. Kwa sasa changamoto anayokabiliana nayo ni mbu.
Akaongeza “Wengine ni wagonjwa na hakuna dawa.”
Hata hivyo kuna matumaini kwenye changamoto za Wakenya walioko kwenye mpaka huo, kwani Serikali ya Kenya sasa inafanya mashauriano na Serikali ya Thailand kuhakikisha kuwa mpaka unafunguliwa tena kwa misingi ya kibinadamu ili kuwaruhusu raia waliokolewa kuingia katika ardhi ya Thailand ili waweze kurejeshwa nyumbani Kenya.
Kenya yahaha kuwasaidia waliokwama warejee nyumbani
Wizara ya Mambo ya Nje ya kenya imesema kuwa Balozi wa Kenya nchini Thailand amekuwa akiwasiliana kila siku na Wakenya walionaswa mpakani huku maafisa wakitafuta njia mbadala za kuwarudisha nyumbani. Wakati huo huo, hali katika kambi za kijeshi za muda zilizoko katika Jimbo la Karen, Myanmar, ambako waathiriwa wanahifadhiwa, bado ni mbaya kwani kuna ukosefu wa huduma za matibabu, maji safi, umeme, na usafi wa mazingira.
Joseph Malevu aliwahi kuwa Mynamar, ila aliokolewa na serikali ya Kenya. Kwa ufupi alizungumzia masaibu ya waathiriwa. “Hawa watu wanafanya kazi ya sulubu, kisha wanapigwa kama hawajatimiza malengo ya siku ya shilingi milioni moja na nusu pesa za kenya, huo ni ulaghai, tuna wakenya wengi ambao wanasuburi kuokolewa. Ni vyema serikali iwarejeshe nyumbani kwa sababu sio kupenda kwao, walikuwa wanatafuta.”
Sikiliza pia:
Serikali imewahimiza Wakenya wanaotafuta ajira nje ya nchi kuhakikisha wanathibitisha mashirika ya ajira na Wizara ya Kazi na pia kuhakiki ofa za kazi za nje na Idara ya Masuala ya Diaspora ili kuepuka kunaswa katika mitego ya ulanguzi wa binadamu.
Wakenya hao ni sehemu ya kundi la zaidi ya watu 7,000 wa mataifa mbalimbali waliokolewa na makundi mawili yenye silaha - Democratic Karen Buddhist Army (DKBA) na Border Guard Force (BGF). Hata hivyo, bado hawajavuka mpaka kuingia Thailand kwa ajili ya kurejeshwa makwao.
Hali hii inatokana na mamlaka za Thailand kutofungua tena mpaka tangu tarehe 12 Februari 2025, ambapo kundi la kwanza la waathiriwa 260, wakiwemo Wakenya 23, walikabidhiwa kwa Jeshi la Kifalme la Thailand na DKBA. Inakadiriwa kuwa zaidi ya waathiriwa 7,000 hao wanatoka katika zaidi ya mataifa 30, yakiwemo ya Amerika Kusini.