Mark Rutte asema Urusi bado ni kitisho kwa NATO
4 Aprili 2025Katika mkutano huo uliolenga kutafuta njia za kuufanya mfungamnao huo wa kijeshi kuwa madhubuti zaidi baadhi ya mawaziri wa Ulaya wameomba Urusi iwekewe siku ya mwisho ya kujibu pendekezo la Marekani la kusitisha vita.
Hata hivyo, Rutte hakuweka wazi kama analiunga mkono pendekezo hilo au la. Katibu Mkuu huyo wa NATO pia amebainisha kuwa washirika wa jumuiya hiyo wataongeza fedha zaidi kwa ajili ya bajeti ya ulinzi na wengi wao wameshaanza kufanya hivyo.
Soma zaidi: Mawaziri wa NATO wajadili mustakabali wa Ukraine
Naye Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio amesema nchi yake itafahamu ndani ya wiki chache kama kweli Urusi ina nia ya dhati ya kupata amani katika mzozo wake na Ukraine.
Amesema, "Kama ni mbinu, Rais Trump hana haja na hilo. Hataingia kwenye mtego wa mazungumzo yasiyo na mwisho. Kama kweli Urusi inataka amani itakuwa vizuri na tutasonga mbele kuelekea kwenye amani. Na kama hawamaanishi tutatathmini msimamo wetu ili kujua ni nini cha kufanya katika hilo".
Uingereza, Ufaransa zamlaumu Putin kwa kukwamisha juhudi za kusitisha vita
Marco Rubio, ameyasema hayo baada ya Uingereza na Ufaransa kumshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuyachelewesha kwa makusudi mazungumzo ya kusitisha vita yanayodhamiria kuumaliza uvamizi wa majeshi yake nchini Ukraine.
Kando na kuuelezea msimamo wa Marekani kuhusu suala hilo Rubio amesema nchi yake inajihusisha na masuala ya Jumuiya ya kujihami ya NATO kuliko wakati mwingine wowote. Akiizungumzia kauli hiyo Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema hakikisho lililotolewa na Marekani lilikuwa na umuhimu mkubwa lakini nchi za Ulaya zinapaswa kuwa imara.