Marekani yazitaka India na Pakistan kupunguza mvutano
1 Mei 2025Kulingana na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani, Marco Rubio amezungumza na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif na Waziri Mambo ya Nje wa India Subrahmanyam Jaishankar kwa nyakati tofauti na kuonesha kuiunga mkono India katika kupambana na makundi yenye itikadi kali.
Soma zaidi: Pakistan yaituhumu India kupanga kuishambulia
Kwa upande mwingine Rubio ameitaka Pakistan kuonesha ushirikiano katika mchakato wa uchunguzi wa shambulio la Aprili 22, 2025 katika jimbo la Kashmir linalogombaniwa na India na Pakistan lililowauwa watu 26 ambapo wengi wao walikuwa watalii.
Katika tukio hilo, kundi la watu wenye itikadi kali za Kiislamu, walilivamia kundi la watu kwenye eneo la Pahalgam na kuwatenga wanawake. Waliwauliza majina yao kisha waliwapiga risasi Wahindu, kulingana na waliosalimika kwenye tukio hilo.
Kuhusu mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Kigeni wa India Subrahmanyam Jaishankar kupitia Ukurasa wake wa X amesema amemwambia Rubio kwamba waliohusika na shambulio hilo, walioliunga mkono na wale waliolipanga ni lazima wafikishwe mbele ya sheria.India inadai kuwa Pakistan ilihusika na tukio hilo suala ambalo Pakistan inalikanusha.
Pakistan yaitaka Marekani iishinikize India ifanye kazi kwa kuwajibika
Naye Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif kupitia ofisi yake ameitaka Marekani kuibana India ili iache kulazimisha kwamba Pakistan ilihusika na tukio hilo na badala yake ifanye kazi kwa kuwajibika.
Mazungumzo hayo yamefanyika muda mfupi baada ya Kiongozi wa jimbo la Kashmir linalozozaniwa Sultan Mahmood Chaundry kutoa wito kwa mataifa kuingilia kati ili kutuliza hali katika mgogoro huo. Alisema kuwa "Tunatarajia usuluhishi kutoka kwa nchi rafiki, na tunatumaini kuwa majadiliano yatafanyika, vinginevyo India inaweza kufanya lolote hivi sasa. "
Wakati huohuo, kuna taarifa kuwa pande mbili za mzozo huo zimeshambuliana kwa risasi usiku wa kuamkia Alhamisi 01.05.2025 huko Kashmir. Kufuatia hali hiyo, mamlaka za jimbo hilo zimetangaza kuzifunga shule za kidini karibu 1,000 kutokana na hofu ya mashambulizi ya kisasi kutoka India.
Mvutano kati ya India na Pakistan unazidi kuongezeka siku moja baada ya serikali mjini Islamabad kusema ina taarifa za uhakika za kiintelijensia kwamba India inapanga kuishambulia ndani ya siku chache zijazo.