Marekani yawawekea vikwazo maafisa 6 wa China na Hong Kong
1 Aprili 2025Marekani imewawekea vikwazo maafisa sita wa vyeo vya juu wa China na Hong Kong katika kile inachokiita kuwa ni ukandamizaji wa kimataifa na kudhoofisha uhuru wa Hong Kong.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza siku ya Jumatatu kuwa watu hao wametumia sheria yenye utata ya usalama wa taifa, sheria ambayo inaipa serikali ya Hong Kong nguvu zaidi kuukandamiza upinzani, kuwalenga wanaharakati wanaounga mkono demokrasia, wakiwemo Wamarekani.
Waliowekewa vikwazo ni pamoja na Dong Jingwei, afisa wa zamani wa ngazi ya juu katika shirika la ujasusi la kiraia la China ambaye sasa anaongoza Ofisi ya Beijing ya Kulinda Usalama wa Taifa huko Hong Kong.
Maafisa wengine waliolengwa katika vikwazo hivyo ni Sonny Au, Dick Wong, Margaret Chiu, kamishna wa polisi wa Hong Kong, Raymond Siu na Paul Lam, katibu wa sheria wa jiji hilo.