Marekani yatishia kuufunga ubalozi mdogo wa Afrika Kusini
21 Machi 2025Hii ni iwapo mamlaka za mji wa Johannesburg zitaendelea na mpango wa kubadilisha jina la barabara iliyopo eneo hilo kwa heshima ya mwanaharakati wa kisiasa wa Kipalestina, Leila Khaled.
Marekani ina wasiwasi kwamba hatua hiyo inaweza kuathiri uhusiano wake na Afrika Kusini, hasa kwa kuwa Khaled anahusishwa na harakati za Palestina ambazo Washington inazizingatia kuwa za kigaidi.
Tayari Rais Cyril Ramaphosa amepanga kufanya mazungumzo na Baraza la mji wa Johannesburg kuhusu athari za kidiplomasia zinazoweza kutokea kutokana na mpango huo wa kubadili jina la barabara inayopita ubalozi mdogo wa Marekani wa Santon.
Soma pia:Marekani yamfurusha balozi wa Afrika Kusini
Iwapo jina la barabara hiyo litabadilishwa, uamuzi huo unaweza kuteteresha zaidi mahusiano kati ya Afrika Kusini na Marekani, ambayo tayari yanakumbwa na msukosuko tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump.
Mnamo wiki za karibuni, Washington imezuia misaada kwa Afrika Kusini ikiituhumu kukiuka haki za binadamu, kupuuza misingi ya utawala bora na kutokana na uungaji wake mkono wa Palestina dhidi ya mshirika ya Israel iliyo mshirika wa karibu wa Marekani.