Marekani yasitisha misaada yote ya kigeni
25 Januari 2025Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio, siku chache baada ya Rais Donald Trump kuchukua madaraka na kuapa kuzingatia sera yake ya kutoa kipaumbele kwa maslahi ya Marekani. Hata hivyo hatua hiyo haiyahusu mataifa ya Israel na Misri.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwa wafanyakazi wa wizara husika, imesema hakuna fedha zitakazotolewa kwa ufadhili mpya ama kuongezwa muda kwa ufadhili uliopo, hadi kila pendekezo jipya la ufadhili litakapotathminiwa na kuidhinishwa upya .
Hata hivyo, Rubio ameagiza kuendelezwa kwa ufadhili wa Marekani kwenye misaada ya dharura ya chakula, ambayo nchi hiyo imekuwa ikichangia kufuatia machafuko duniani kote ikiwa ni pamoja na Sudan na Syria. Mwaka 2023, Marekani ilitoa misaada ya maendeleo ya zaidi ya dola bilioni 64.