Marekani yasitisha misaada ya kijeshi kwa Ukraine
2 Julai 2025Kila upande unatafuta kuibuka kuwa na nguvu kuliko upande mwingine kabla ya kuanza msimu wa mapukutiko, wachambuzi na makamanda wa kijeshi wanasema Urusi inalenga kuongeza mafanikio yake kwa kudhibiti maeneo zaidi ya Ukraine kabla ya kuzingatia usitishaji kamili wa mapigano.
Ukraine kwa upande wake inataka kuzuia kasi ya Urusi ya kusonga mbele kwa kipindi cha muda mrefu iwezekanavyo na kuisababishia Urusi hasara kubwa. Hata hivyo vikosi vya Urusi vimezidi kupata nguvu na vinalenga kulidhibiti eneo la Pokrovsk, la kimkakati lililopo mashariki mwa Ukraine hatua ambayo inakaribia kuyawezesha majeshi ya Urusi kuliteka eneo lote la Donetsk.
Huku hayo yakiendelea, Marekani imesema inasitisha kupeleka baadhi ya silaha muhimu nchini Ukraine ambazo ziliahidiwa chini ya utawala wa Rais Joe Biden, kwa ajili ya kuisaidia Ukraine katika vita vyake na Urusi.
Soma pia: Urusi yaendelea kuchukua udhibiti wa maeneo nchini Ukraine
Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa uamuzi huu umechukuliwa kwa ajili ya kuifanikisha sera ya ‘Marekani Kwanza' . Naibu Katibu wa Habari wa White House, Anna Kelly, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kupokea tathmini ya Idara ya Ulinzi, DOD.
Amesema kupunguzwa kwa misaada ya kijeshi kunaashiria mabadiliko katika vipaumbele vya Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye anazishinikiza Urusi na Ukraine kuharakisha mazungumzo ya amani yaliyokwama.
Raia wa Ukraine wameitaja hatua ya kusitisha misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine, wamesema ni ya kukatisha tamaa.
Soma zaidi: Urusi yafanya mashambulizi makubwa dhidi ya Ukraine
Wiki iliyopita katika mkutano wa wa kilele wa Jumuiya kujihami ya NATO, uliofanyika nchini Uholanzi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, alikutana na Trump lakini hakupata majibu yaliyoeleweka kutoka kwa kiongozi huyo wa Marekani kuhusu mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot.
Kusitisha kuipa Ukraine silaha na misaada mingine ya kijeshi ikiwa ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga ni pigo kwa Ukraine wakati inapokabiliana na mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Urusi katika vita hivyo vilivyoingia katika mwaka wa tatu sasa.
Vyanzo: AFP/AP