Marekani yasitisha kuchangia kikosi cha kulinda amani Haiti
5 Februari 2025Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema Jumatano kuwa kiasi hicho cha fedha kilitarajiwa kutolewa kwa kikosi hicho kinachoongozwa na Kenya, ambacho tayari kinapokea ufadhili mdogo wa kifedha. ''Kwa upande wa Haiti, tumepokea taarifa rasmi kutoka Marekani, ikiomba kusitishwa mara moja mchango wake katika kikosi cha kimataifa cha kulinda amani,'' alifafanua Dujarric.
Marekani iliahidi dola milioni 15
Dujarric amewaambia waandishi habari kwamba Marekani iliahidi kutoa dola milioni 15 katika mfuko huo, ambapo dola milioni 1.7 tayari zimeshatolewa na kutumika, hivyo dola milioni 13.3 sasa zimesitishwa.
Hatua ya Marekani kusitisha ufadhili wake ni sehemu ya shinikizo la Rais Donald Trump kupunguza misaada ya Marekani nje ya nchi, harakati ambazo zimejumuisha kuzifunga shughuli za shirika kuu la misaada la serikali, USAID.
Oktoba mwaka 2023, Umoja wa Mataifa uliidhinisha kupelekwa kwa kikosi hicho cha kimataifa ili kuwasaidia viongozi wa Haiti kupambana na magenge ya wahalifu, ambao wanayadhibiti maeneo mengi ya nchi hiyo.
Hata hivyo, licha ya kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kikosi hicho cha kimataifa sio operesheni ya Umoja wa Mataifa na kwa sasa kinategemea michango ya hiari. Hadi sasa, kikosi hicho kimepiga hatua kidogo sana kuisaidia Haiti kurejesha utulivu.
Askari 900 wanahudumu Haiti
Kuna takribani polisi na wanajeshi 900 kutoka Kenya, El Salvador, Jamaica, Guatemala na Belize. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya dola milioni 110 zimetolewa katika mfuko wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ujumbe huo, huku zaidi ya nusu ya fedha hizo zikitolewa na Canada.
Mwishoni mwa mwezi Januari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alionya kuwa mji mkuu wa Haiti, Port-Au-Prince huenda ukaangukia mikononi mwa magenge ya wahalifu iwapo jumuia ya kimataifa haitoongeza msaada wake katika kikosi hicho cha kulinda usalama Haiti.
Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti, Jean-Victor Harvel Jean-Baptiste amesema nchi yake inakabiliwa na matatizo makubwa ambayo sio tu yanautatiza umma, bali pia yanatishia uhai na usalama wa nchi hiyo.
Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Korir Sing'Oei amesema hadi sasa mfuko huo umepokea dola milioni 83 kutoka kwa nchi kadhaa zilizoahidi kuchangia, ikiwa ni pamoja na kiasi kikubwa kutoka kwa Marekani.
Wanajeshi wa El Salvador wajiunga na kikosi
Wakati huo huo, wanajeshi wa El Salvador Jumanne wamejiunga na kikosi hicho katika kupambana na ghasia zinazofanywa na magenge ya wahalifu ambayo yaliwaua maelfu ya watu mwaka uliopita na kuchukua udhibiti kwenye maeneo mengi ya mji mkuu.
Wanajeshi 70 wa El Salvador watatumia utaalamu wao katika usaidizi wa anga, jambo ambalo maafisa wa Kenya wamesema litakuwa muhimu sana kwa ajili ya kuwaokoa na kuwasafirisha watu wanaohitaji kupatiwa matibabu.
(AFP, AP, Reuters)