Marekani yashinikiza makubaliano ya amani Rwanda, Kongo
13 Juni 2025Mjumbe maalum ya Marekani kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, Troy Fitrell, amesema timu za ufundi zinalifanyia kazi suala hilo kwa sasa na kwamba mara hii hakutakuwa tena na kurudi nyuma.
Mkutano uliopangwa kufanyika mwezi Mei kati ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda na Kongo haukufanyika, huku pande hizo mbili zikizidi kulaumiana kwa kuuhujumu mchakato huo unaosimamiwa na Marekani.
Soma zaidi: Rwanda yajiondoa katika Jumuiya ya ECCAS kufuatia mzozo na DRC
Katika juhudi nyengine zinazosimamiwa na Qatar, wawakilishi wa Kinshasa na kundi la waasi la M23 wanatazamiwa kuelekea mjini Doha ndani ya wiki hii kwa mashauriano.
Licha ya juhudi za kikanda na kimataifa, hali ya kutoaminiana kati ya Kinshasa na Kigali imekuwa ikizuwia kupatikana kwa mkataba wa amani, huku Kongo ikiishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 waliotwaa eneo kubwa la mashariki mwa Kongo katika miezi ya hivi karibuni.