Marekani yasema wakfu mpya utapeleka misaada Gaza
9 Mei 2025Matangazo
Marekani imesema wakfu mpya utatangaza hivi karibuni mipango ya upelekaji wa msaada Gaza, kuuweka kando Umoja wa Mataifa huku hatua ya Israel kuzuia misaada kwa miezi miwili ikisababisha uhaba mkubwa katika eneo hilo linalokabiliwa na vita.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tammy Bruce amesema wakfu huo si wa kiserikali na utatoa tangazo hilo karibuni bila kutoa maelezo zaidi.
Wakati hayo yakiarifiwa jeshi la Israel limesema katika taarifa kwamba wanajeshi wake wawili wameuwawa kwenye mapambano kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Awali hapo jana kundi la Hamas lilisema wanamgambo wake walikuwa wakipambana katika mapigano makali na wanajeshi wa Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza karibu na Rafah.