Marekani: Trump, Putin na Zelensky Kukutana Alaska?
11 Agosti 2025Makamu wa Rais JD Vance wa Marekani amesema Marekani ipo katika jitihada ya kupanga mkutano kati ya Donald Trump na viongozi wenzake wa Urusi na Ukraine, katika kipindi hiki ambacho pia washirika wa Ukraine kwa Ulaya wakisisitiza Kyiv ihusishwe katika mkutano wa kilele kati ya Marekani na Urusi utakaofanyika Alaska juma hili.
JD Vance amesikika katika mahojiano maalumu katika kipindi cha Asubuhi ya Jumapili ya kituo cha "Fox News akisema "Moja ya vikwazo muhimu zaidi ni kwamba Vladimir Putin alisema hatokaa meza moja na Volodymyr Zelensky, kiongozi wa Ukraine, lakini sasa rais ameweza kubadilisha msimamo huo."
Alipoulizwa kuhusu matarajio yake kwa mkutano wa kilele wa Alaska tarehe 15 Agosti alisema kwamba wao, wapo katika hatua ya kujaribu, kupanga ratiba na mambo mengine yanayohusiana na lini viongozi hawo watatu wanaweza kukutana na kujadili njia ya kumaliza mgogoro huo. Makamu wa Rais aliongeza kwa kusema kuwa Marekani inajaribu "kutafuta suluhisho la mazungumzo ambalo Warusi na Waukraine wanaweza kukubaliana nalo."
Hofu ya Ulaya kwa mkutano wa Trump na Putin
Mkutano wa kilele kati ya Marekani na Urusi uliopangwa kufanyika Alaska bila uwepo wa Rais Volodymyr Zelensky umeibua wasiwasi, kwamba makubaliano yoyote yanaweza kumlazimisha Ukraine kukubali kupoteza maeneo ya ardhi, jambo ambalo Umoja wa Ulaya unalipinga vikali.
Katika juhudi za kidiplomasia, Rais Volodymyr Zelensky alifanya mazungumzo ya simu na viongozi 13 ndani ya kipindi cha siku tatu, wakiwemo washirika wakuu wa Kyiv kama vile Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.
Awali Jana Jumapili Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema kuwa anatumaini na anaamini kwamba Zelensky atahudhuria mkutano huo wa kilele. Akizungumza na kituo cha televisheni cha ARD angalifanya mazungumzo kwa kwa njia ya simu na Trump na kwamba kwa upande wao wanajiandaa kwa kina katika ngazi ya Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya Marekani kwa ajili ya mkutano huo.
Lengo la Trump kwa amani ya Ukraine
Na kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte, amesema kwamba mazungumzo ya amani yajayo kuhusu vita vya Ukraine huenda yatalazimika kushughulikia hatma ya maeneo ambayo kwa sasa yako chini ya udhibiti wa Urusi. "Imani yangu thabiti kwa siku ya Ijumaa ni kwamba huu ni mpango wa Rais Trump wa kuhakikisha kuwa Putin anamaanisha. Na kama hatomaanisha, basi utaishia hapo. Lakini kama atakuwa na nia ya kweli, basi kuanzia Ijumaa mchakato utaendelea. Ukraine itahusishwa, Ulaya itahusika, na Marekani tayari inaratibu."
Katika maeneo ya mapambano hapo Jumapili, mashambulizi mapya ya Urusi yaliofanyika kwa mizinga na droni yalisababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine kadhaa nchini Ukraine, hasa katika maeneo ya Donetsk, Zaporizhzhia, na Kherson. Katika mji wa Zaporizhzhia, bomu la Urusi lililenga kituo cha mabasi kilichojaa watu, na kujeruhi watu 19 kwa wakati mmoja.
Wakati huo huo, Ukraine ilifanya mashambulizi ya droni ndani ya Urusi, ikilenga viwanda viwili vya kusafisha mafuta vilivyoko Saratov na Ukhta. Lakini pia kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka ya Urusi mtu mmoja ameuawa katika eneo la Nizhny Novgorod nchini humo kutokana na mashambulizi ya droni ya Ukraine.