Marekani yaonya kuhusu udhibiti wa Akili Mnemba
11 Februari 2025Akizungumza Jumanne mjini Paris katika mkutano wa kilele kuhusu Akili Mnemba, kwa niaba ya Rais Donald Trump, Vance amesema wana amini kuwa kanuni kali katika sekta ya Akili Mnemba zinaweza kuua moja ya teknolojia nyingi ambayo inaonyesha dalili za mafanikio ya baadae ambayo imeshuhudiwa katika vizazi. Aidha, amewatolea wito viongozi wa Ulaya kuonyesha matumaini badala ya hofu.
Kulingana na Vance, ulimwengu uko kwenye hatihati ya mapinduzi mapya ya viwanda, na hotuba yake imeashiria mpasuko mkubwa wa pande tatu kuhusu mustakabali wa teknolojia hiyo.
Usalama wa Akili Mnemba
Marekani, chini ya Rais Trump, inashikilia mbinu ya uhuru katika kuchochea uvumbuzi, wakati Ulaya inaimarisha udhibiti wake kwa kanuni kali ili kuhakikisha usalama na uwajibikaji.
Wakati huo huo, China inatanua kwa kasi teknolojia ya Akili Mnemba kupitia makumpuni makubwa ya teknolojia yanayoungwa mkono na serikali, yakiwania kutawala kimataifa.
Matamshi ya Vance, hayakuyazuia mataifa kadhaa kusaini hati inayotaka juhudi za kuiwekea teknolojia hiyo kanuni ili kuifanya iwe ya ''wazi'' na yenye ''maadili''. Marekani haikuonekana katika hati ya kimataifa iliyosainiwa na zaidi ya mataifa 60, ikiwa ni pamoja na China, na kuufanya utawala wa Trump kuwa tofauti katika ahadi ya kimataifa ya kukuza maendeleo ya kuwajibika kuhusu Akili Mnemba.
Akili Mnemba kulinda taarifa za watumiaji
Hati hiyo ya pamoja imeahidi kuimarisha upatikanaji wa teknolojia ya Akili Mnemba ili kupunguza migawanyiko ya kidijitali, na kuhakikisha Akili Mnemba iko wazi, inajumuisha, salama na ya kuaminika. Makubaliano hayo pia yametaka kuifanya Akili Mnemba kuwa endelevu kwa watu, na kulinda haki za binadamu, usawa wa kijinsia, lugha, mchanganyiko wa watu, kulinda taarifa za watumiaji na haki miliki.
Kwa upande wake, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuna haja ya kuwepo sheria na mfumo wa kuaminika kuhusu maendeleo ya Akili Mnemba. Macron amesema sekta ya Akili Mnemba inahitaji sheria katika ngazi ya kimataifa, ili watu waweze kuiamini teknolojia hii mpya.
''Tunapaswa, kama tulivyofanya kwenye mkutano huu wa kilele, kuendelea kusonga mbele katika utawala wa kimataifa wa Akili Mnemba. Kwa kuzingatia miungano yetu tunayoizindua leo, itaturuhusu kuunganisha vipengele vya uaminifu katika Akili Mnemba kwa sababu tunahitaji kuweka sheria, ili kuhakikisha tunaaminiana. Sio kutoaminiana,'' alifafanua Macron.
Wakati huo huo Uingereza imeelezea maslahi ya kitaifa kwa nchi hiyo kutosaini taarifa ya mwisho katika mkutano wa kimataifa wa Akili Mnemba. Msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema kwamba majadiliano yanaendelea na kwamba Uingereza inaungana na juhudi za mipango mingine na itaendelea kushirikiana na washirika wake ikwiemo Ufaransa. Amesema watasaini tu mipango yenye maslahi ya kitaifa ya Uingereza.
Soma zaidi: Kongamano la Akili Mnemba
Ama kwa upande mwingine, ofisi ya rais wa Ufaransa imesema kuwa India itakuwa mwenyeji ajaye wa mkutano wa kimataifa kuhusu Akili Mnemba baada ya kuandaa kwa pamoja na Ufaransa, mkutano wa Paris Jumatatu na Jumanne. Awali, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliwaambia washiriki wa mkutano wa Paris kwamba India itafurahi sana kuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa Akili Mnemba katika ardhi yake.
(AFP, AP, DPA, Reuters)