Marekani yalegeza msimamo wake kuhusu kuichukua Gaza
6 Februari 2025Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema uhamisho wa wakaazi wa Gaza utakuwa wa muda.
"Na jambo pekee ambalo Rais Trump amefanya – kwa ukarimu mkubwa, kwa mtazamo wangu – ni kuonyesha utayari wa Marekani kuingilia kati, kuondoa vifusi, na kuisafisha Gaza kutokana na uharibifu wote uliopo. Pia, kusafisha eneo hilo dhidi ya mabomu ambayo hayajalipuka. Wakati huo huo, watu wanaoita Gaza nyumbani hawataweza kuishi hapo wakati vikosi vinaendelea kuondoa mabaki na silaha hizo. Hilo ndilo pendekezo alilotoa," alisema Rubio.
Guterres alikataa pendekezo la Trump kuhusu Gaza
Awali, Trump alisema Marekani itauchukua Ukanda wa Gaza kwa ujenzi mpya. Hata hivyo, Msemaji wa Ikulu Karoline Leavitt amesema Washington haitafadhili ujenzi huo baada ya miezi 15 ya vita kati ya mshirika wake Israel na Hamas. Amebainisha kuwa ushiriki wa Marekani hautahusisha kutuma wanajeshi wala kutumia kodi za Wamarekani kufadhili mpango huo.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema leo kuwa ameliamuru jeshi kutengeneza mpango wa kuwawezesha Wapalestina kuondoka Gaza. Amesema mpango huo utamuwezesha mkaazi yeyote kutoka Gaza anayetaka kuondoka kwa hiari, kufanya hivyo, kwa nchi yoyote iliyo tayari kuwakubali.