Marekani yamfukuza balozi wa Afrika Kusini
15 Machi 2025Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amesema Marekani inamfukuza balozi wa Afrika Kusini mjini Washington Ebrahim Rasool. Akizungumza hapo jana Rubio alimtuhumu balozi huyo kwa kuichukia Marekani na rais Donald Trump.
Rubio aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba balaozi wa Afrika Kusini nchini Marekani hakaribishwi tena katika nchi yao na hawana la kujadili naye.
Kufukuzwa kwa balozi Rasool, hatua ya nadra kuchukuliwa na Marekani, ni tukio la hivi karibuni kabisa la ongezeko la msuguano kati ya serikali ya mjini Washington na ile ya mjini Pretoria.
Febrauri mwaka huu Trump alisitisha msaada kwa Afrika Kusini akitaja sheria nchini Afrika Kusini ambayo anadai inaruhusu ardhi kutekwa kutoka kwa wakulima weupe.
Wiki iliyopita Trump alichochea zaidi hali ya wasiwasi akisema wakulima wa Afrika Kusini wanakaribishwa kwenda kuishi Marekani baada ya kurudia madai yake kwamba serikali inachukua kwa nguvu ardhi kutoka kwa watu weupe.