Marekani yaliwekea vikwazo kundi la Pareco-FF la DRC
13 Agosti 2025Washington imetangaza kuzuia mali za kundi linalofahamika kama Coalition des Patriotes Resistants Congolais-Forces de Frappe (Pareco-FF), kikundi chenye silaha kinachopambana pia na M23 inayoungwa mkono na Rwanda.
Aidha, kampuni ya uchimbaji madini ya Kongo na makampuni mawili ya Hong Kong yamewekewa pia vikwazo kwa tuhuma za kununua madini kutoka kwa kundi hilo lenye silaha.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Tammy Bruce amesema katika taarifa kuwa Marekani inatuma ujumbe ulio wazi kuwa hakuna kikundi chenye silaha au taasisi ya kibiashara isiyoweza kuwekewa vikwazo ikiwa vitachangia kuvuruga amani, utulivu na usalama nchini Kongo.
Kundi la Pareco-FF lina ushawishi mkubwa huko Rubaya , mashariki mwa DRC, kunakochimbwa kati ya asilimia 15 na 30 ya madini ya Coltan kote duniani, ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta na simu za mkononi.