Marekani yalegeza vikwazo dhidi ya Iran:
1 Januari 2004Matangazo
WASHINGTON: Marekani imelega vikwazo vyake dhidi ya Iran ili kuchangia harakati za kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa baada ya mtetemeko mkubwa wa ardhi. Watoa michango ya hiyari na mashirika ya kukusanya michango ya pesa na misaada ya kiutu wamepewa muda wa siku 90 kuyapelekea misaada mashirika yasio ya kiserikali nchini Iran, ikiwa imethibitika kuwa mashirika hayo yanashiriki katika ukarabati na usambazaji wa misaada ya kiutu nchini humo. Pamoja na hayo mashirika ya misaada yatalegezewa masharti ya kuingiza simu za satalaiti na kompyuta nchini Iran. Maafisa wa Iran wamearifu kuwa katika eneo lililoshambuliwa na mtetemeko wa ardhi watu wapatao laki moja wamepoteza maskani yao katika mkoa wa maafa wa Kerman. Kwa mujibu wa makisio rasmi watu wapatao 30,000 wameuawa katika balaa hilo kubwa.