Marekani yakanusha kuisaliti Ukraine
13 Februari 2025Awali Umoja wa Ulaya ulisisitiza kwamba Ukraine na mataifa mengine ni lazima wawepo katika meza ya mazungumzo ya kumaliza vita hivyo isiwe ni mazungumzo ya kipekee kati ya Trump na Putin. Hegseth amesema hakuna usaliti wa aina yoyote uliojitokeza wakati Trump alipozungumza kwa njia ya simu na rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye Trump alisema kiongozi huyo wa Urusi alionyesha nia ya kumaliza vita nchini Ukraine.
''Hakuna usaliti hapo, kuna utambuzi kwamba dunia nzima pamoja na Marekani inataka amani, majadiliano ya amani na hilo linahitaji pande zote mbili kutambua mambo wasioyoyataka. Ndio maana nasema dunia ina bahati kumpata rais kama Trump ni yeye tu kwa wakati huu anayeweza kuzileta pande zote mbili pamoja kwa ajili ya amani na hiyo ni ishara nzuri,'' alisema Pete Hegseth.
Trump: Tunapiga hatua katika mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine
Hapo jana Jumatano Trump aliitenga Ukraine pamoja na washirika wake wa Ulaya kwa kukubali kuanzisha mazungumzo ya amani na Putin. Hegseth hata hivyo, alionyesha msimamo wa Marekani kwa kusema haiingii akilini kwa Ukraine kudhibiti tena ardhi yake yote au kuwa mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO. Aliongeza kuwa sasa ni wakati wa Ulaya kuendelea kuisaidia zaidi Ukraine na kwamba Marekani haitoüpeleka wanajeshi wake huko kama sehemu ya hakikisho la usalama.
Ujerumani yakosoa makubaliano ya Marekani na Urusi kuhusu amani ya Ukraine
Ujerumani kupitia waziri wake wa ulinzi Boris Pistorius imesema inasikitika kwamba Marekani, imekuwa na makubaliano na Urusi hata kabla mazungumzo ya amani kuanza. Amesema kwa maoni yake masuala ya uanachama wa Ukraine kwa Nato au masuala ya udhibiti wa miji ni mambo yaliyopswa kujadiliwa katika mazungumzo hayo.
Washirika watano wa Ulaya wanatafuta kuimarisha sekta ya silaha ya Ukraine
Hapo jana (12.02.2025), taarifa ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa kadhaa barani Ulaya ikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Poland, Sweden, Estonia na Uingereza walisema Ukraine na Ulaya zinapaswa kuwa sehemu ya majadiliano yoyote ya kusitisha vita baina ya Kiev na Moscow. Mataifa yanayoiunga mkono Ukraine yana wasiwasi kwamba Trump huenda akailazimisha Ukraine kukubali makubaliano mabaya ya amani yatakayompendelea Rais Putin.
Kwa upande wake Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza lililo na nguvu la Usalama nchini Urusi amesema maongezi kati ya Trump na Putin yanaonyesha kuwa nia ya Ulaya ya kutaka kuishinda Urusi haitawahi kufanikiwa. China nayo kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje, Guo Jiakun imesema inafurahi kuiona Marekani na Urusi zikiimarisha mawasiliano yao juu ya masuala tofauti ya kimataifa.
dpa/reuters/ap