Marekani yajiandaa kwa maandamano makubwa dhidi ya Trump
14 Juni 2025Miji mikubwa kwa midogo inajiandaa kwa maandamano makubwa leo nchini Marekani dhidi ya Rais Donald Trump, huku maafisa wakitoa wito wa utulivu. Rais Trump anatarajiwa kuhudhuria gwaride la kijeshi mjini Washington kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 250 ya jeshi la nchi hiyo.
Maandamanoyaliyopachikwa jina la "No Kings" yaani "Hatutaki Wafalme" yamepangwa kufanyika jijini Philadelphia, lakini hakuna matukio yaliyopangwa huko Washington, ambako gwaride hilo la kijeshi linafanyika huku likirandana na siku ya kuzaliwa ya Trump.
Maandamano hayo ni mwendelezo wa maandamano yaliyozuka kote nchini humo kutokana na utekelezaji wa amri ya kuwatimua wahamiaji ilioanza wiki iliyopita, na pia agizo la Trump la kuwatuma askari wa jeshi la kitaifa na wale wa jeshi la wanamaji huko Los Angeles. Waandamanaji walifunga barabara na kuchoma magari.