Marekani yajadili na Urusi kuhusu madini yake
31 Machi 2025Urusi na Marekani zinajadili uwezekano wa kuwa na ushirikiano katika miradi ya madini adimu ya chuma ya Urusi, hayo ni kulingana na kauli rasmi iliyotolewa na Kirill Dmitriev, mkuu wa hazina ya utajiri wa Urusi. Afisa huyo mkuu amesema kampuni kadhaa tayari zimeonyesha nia kutaka kushiriki kwenye mradi huu, ingawa hakutoa maelezo zaidi. Madini hayo adimu ni muhimu sana katika utengenezaji wa bidhaa zinazohusisha teknolojia ya kisasa kama simu za kisasa, kompyuta mpakato na hata magari ya umeme.
Soma pia: Ukraine yaripoti mapigano makali Donbass
Dmitriev anaongoza Mfuko wa Uwekezaji wa Moja kwa moja wa Urusi na ni mtu muhimu katika mazungumzo ya Moscow na Washington juu ya kuurekebisha uhusiano wa pande hizo mbili. Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kuurekebisha uhusiano uliozorota kati ya nchi yake na Urusi na kuvimaliza vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Wakati huo huo Urusi imefanya mashambulizi usiku wa kuamkia leo yakiwa ni mashambulizi yalioendelea kwa siku ya pili mfululizo katika mji wa Kharkiv ulioko kaskazini mashariki mwa Ukraine. Watu watatu wamejeruhiwa, na yamesababisha moto kuwaka katika majengo kadhaa ya viwanda. Maafisa wa Ukraine wameripoti kwamba shule mbili za chekechea pia zimeharibiwa vibaya.
Meya wa jiji la Kharkiv Ihor Terekhov amesema mashambulizi ya Urusi kwenye, mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, yameilenga wilaya moja kongwe katika jiji hilo. Meya Terekhov amesema majengo matano ya viwanda na moja la kufanyia utafiti na uzalishaji wa bidhaa za kibiashara yameharibiwa.
Soma pia: Putin apendekeza utawala wa mpito Ukraine
Wafanyakazi wa idara ya kukabiliana na dharura wamesema walipambana na moto mkubwa ambao uliteketeza eneo la mita za mraba 3,900 baada ya mashambulio hayo ya Urusi. Wamesema mashambulio hayo ya droni pia yameharibu majengo ya ghorofa 11 ya makazi ya watu. Rais Volodymir Zelensky ameitaka Marekani na washirika wa Ukraine kuongeza shinikizo kwa Urusi ili kuvunja uwezo wa nchi hiyo wa kuendeleza vita.
Urusi imefanya mashambulio hayo wiki moja tu baada ya Marekani kusimamia usitishaji wa vita kwa muda dhidi ya miundombinu katika Bahari Nyeusi. Pande zote mbili za Urusi na Ukraine zinashutumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha vita.
Vyanzo: Rtre/Dpa