Marekani yaitetea Israel kuzuia misaada kuingia Gaza
30 Aprili 2025Wakili kutoka wizara ya mambo ya nje ya Marekani Josh Simmons, ameiambia mahakama ya ICJ kwamba Israel ina maslahi halali ya kiusalama kwa kuzuia misaada hiyo ya kibinadamu.
Simmons ameongeza kuwa Marekani inaunga mkono kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu ndani ya Gaza lakini kwa tahadhari kwamba misaada hiyo haitatumiwa vibaya na kundi la kigaidi.
Hatua ya Israel kuzuia misaada Gaza ndio kiini cha kesi iliyoanza wiki hii mjini Hague, Uholanzi.
Soma pia: Uturuki kujiunga kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel
Mahakama hiyo ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa inatarajiwa kutoa ushauri kuhusu wajibu wa kisheria wa Israel wa "kufanikisha na kuruhusu" misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa dharura kwa raia wa Wapalestina.
Kesi hiyo pia inahusisha marufuku ya Israel kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA. Tangu Machi 2, Israel imezuia kuingizwa misaada ya kibinadamu kwa takriban wakaazi milioni 2.1 katika ukanda wa Gaza.