Marekani yafuta kusimamisha msaada kwa ujumbe wa Haiti
6 Februari 2025Tangazo hilo limetolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, akiwasili katika Jamhuri ya Dominika, ambapo atajadili hali ya Haiti. Nchi hiyo imekuwa chanzo kikuu cha uhamiaji, jambo ambalo Rais Donald Trump analenga kudhibiti ili kupunguza wimbi la wahamiaji wanaoingia Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema Rubio amethibitisha msaada wa dola milioni 40.7 kusaidia Polisi ya Taifa ya Haiti na kikosi cha kimataifa cha usalama kinachojumuisha mataifa mbalimbali.
Jumanne wiki hii, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa Marekani ilitoa taarifa ya kusitisha mchango wa dola milioni 13.3 uliotengwa kwa msaada wa Haiti. Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haikukanusha kusitishwa kwa fedha hizo, ikisema ni sehemu ya marekebisho ya mchango wake wa jumla.
Marekani imetoa zana za kijeshi kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya
Aidha, katika wiki hii, Marekani imewasilisha zana nzito za kijeshi kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya pamoja na polisi wa Haiti. Hata hivyo, Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema Umoja huo bado unasisitiza haja ya Haiti kupokea msaada zaidi.
"Wenzetu wa mpango wa kisiasa nchini Haiti wametoa ripoti yao ya hivi karibuni kuhusu haki za binadamu, ikihusisha kipindi cha Oktoba hadi Desemba. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takriban watu 1,732 waliuawa na zaidi ya 400kujeruhiwa kutokana na ghasia za magenge, mashambulizi ya vikundi vyenye silaha, au operesheni za polisi. Hii inafanya jumla ya vifo kwa mwaka uliopita kufikia watu 5,626, huku zaidi ya 2,200 wakijeruhiwa."
Ripoti hiyo pia inaelezea wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana, yanayofanywa na wanachama wa magenge ya uhalifu.
Hofu ya watoto kuandikishwa katika makundi wa wapiganaji Haiti
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema ripoti hiyo inaonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu magenge hayo kuwaandikisha watoto katika mapigano. Aidha, magenge hayo yanaendelea kuziba njia kuu zinazoingia na kutoka jijini Port-au-Prince, na kusababisha vikwazo kwa watu na magari.
Utawala wa Rais wa zamani Joe Biden ulijaribu kuanzisha jeshi la kimataifa kama sehemu ya juhudi za kurejesha utulivu nchini Haiti, ambako magenge ya wahalifu yalidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince.
Soma zaidi: Marekani yasitisha mchango kwa kikosi cha amani Haiti
Serikali ya Biden ilitoa msaada wa kifedha na vifaa lakini haikutuma wanajeshi wa Marekani, huku Kenya ikiongoza operesheni za usalama ndani ya Haiti. Hata hivyo, juhudi hizo zimeingia matatani baada ya Donald Trump kuchukua uongozi na kutoa maagizo ya kupunguza ufadhili wa Marekani kwa mataifa yenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na kufunga baadhi ya shughuli za shirika la misaada la USAID.