Marekani yaendeleza mashambulizi dhidi ya waasi wa Kihouthi
29 Machi 2025Marekani imeendeleza mashambulizi yake ya anga katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa usiku wa kuamkia leo Jumamosi na kuua mtu mmoja. Marekani katika taarifa yake imesema mashambulizi ya hivi karibuni yamelenga moja ya ngome muhimu ya waasi wa Kihouthi katika mji huo.
Taarifa ya kiwango kamili cha uharibifu na uwezekano wa majeruhi hazikuwekwa wazi mara moja, ingawa mashambulizi haya yanafuatia yale yaliyofanyika mapema siku ya Ijumaa na yaliyotajwa kuwa makali zaidi ikilinganishwa na siku nyingine katika hatua za Marekani za kuwashambulia waasi wa Kihouthi zilizoanza Machi 15 mwaka huu.
Soma zaidi.Tetemeko kubwa latikisa Myanmar na Thailand na kuua zaidi ya watu 150
Uchambuzi washirika la habari la AP umebaini kwamba operesheni hii mpya ya Marekani chini ya utawala wa rais Donald Trump ni kubwa zaidi kuliko operesheni za mtangulizi wake Joe Biden.
Kampeni hii mpya ya mashambulizi ya anga ambayo Wahouthi wanasema imeua takriban watu 58, ilianza baada ya waasi hao kutishia kuanza kuzilenga meli katika bahari ya shamu ili kuonyesha uungaji wao mkono kwa Wapalestina wanaopitia madhila ya vita.