Marekani yatekeleza agizo la ushuru dhidi ya Canada, Mexico
4 Machi 2025Agizo la kuzitoza ushuru bidhaa za Mexico na Canada linaloanza kutekelezwa Jumanne 04.03.2025 linatazamiwa kuathiri pakubwa sekta muhimu zikiwemo za magari na vifaa vya ujenzi. Hatua ya kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo la Trump imezua hofu ya uwezekano wa kuibuka kwa mfumuko mkubwa wa bei na vita kubwa ya kibiashara licha ya ahadi ya kiongozi huyo kwa Wamarekani kuwa kodi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo ndiyo njia rahisi zaidi ya taifa hilo kupata Mafanikio.
Ushuru dhidi ya Mexico na Canada ulipangwa kuanza kutekelezwa mwezi Februari lakini Trump alikubali kusitisha hatua hiyo kwa siku 30 ili kufanya majadiliano zaidi na nchi hizo ambazo ni washirika wakubwa wa kibiashara wa Marekani.
Soma zaidi: Trump asema Wamarekani wataumia katika vita vya biashara na Canada, China na Mexico
Sababu za Marekani kuzitoza ushuru bidhaa za Mexico na Canada zinatajwa kuwa ni kupambana na tatizo la ulanguzi wa dawa za kulevya, kupambana na uhamiaji haramu wakati nchi hizo mbili zikisema kuwa zimepiga hatua katika kushughulikia changamoto hizo.
Ieleweke kuwa, asilimia 63 ya bidhaa za mboga mboga na karibu nusu ya matunda na jamii ya karanga zinazoingizwa Marekani zinasafirishwa kutoka Mexico. Pia, Marekani inaingiza vifaa vya ujenzi kutoka Canada hatua inayomaanisha kuwa ushuru ulioanza kutozwa unaweza kupandisha gharama za ujenzi.
Bidhaa za China nazo zaongezewa ushuru
Katika hatua nyingine Donald Trump amesaini agizo la kuongeza zaidi ushuru kwenye bidhaa za China. Awali alitangaza ushuru wa asilimia 10 na sasa ameongeza hadi asilimia 20 kwenye bidhaa mbalimbali kutoka China.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya kigeni ya China Lin Jian, amejibu uamuzi huo wa Trump akisema kuwa, "Tunaishauri Marekani iweke pembeni tabia yake ya uonevu na irejee katika njia sahihi ya mazungumzo na ushirikiano mara moja."
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amesema nchi yake itaanzia kuzitoza ushuru wa asilimia 25 bidhaa zinazoagizwa kutoka Marekani. Naye Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amesema taifa lake lina mipango ya dharura ili kukabiliana na ushuru wa Marekani.