Marekani, Wahouthi waapa kuendelea kushambuliana
17 Machi 2025Wizara ya Afya ya Yemen inayodhibitiwa na kundi la Ansarullah, ama Wahouthi kama wafahamikavyo na wengi, ilisema mashambulizi ya Marekani yaliuwa watu 53, wakiwemo wanawake watano na watoto wawili, na kuwajeruhi wengine takribani 100 kwenye mji mkuu, Sanaa na majimbo mengine, likiwemo jimbo la Saada, ambalo ni ngome ya kundi hilo kwenye mpaka wake na Saudi Arabia.
Akizungumza na televisheni ya CBS siku ya Jumapili (Machi 16), Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, alisema mashambulizi ya nchi yake dhidi ya kundi hilo yangeendelea "hadi pale litakapokuwa halina tena uwezo wa kuzuwia meli kupita kwenye bahari hiyo."
Soma zaidi: Mashambulizi ya Marekani huko Yemen yaua watu 31
Siku moja kabla, Rais Donald Trump alikuwa ameapa kutumia kile alichosema ni "nguvu kubwa kabisa dhidi ya Wahouthi" na wakati huo huo kuionya Iran kuwa ingelibeba dhamana kikamilifu kwa vitendo vyao.
Wahouthi wasema pigo kwa pigo
Kwa upande wao, viongozi wa kundi la Ansarullah nao waliapa kuziandama meli za kijeshi na mizigo za Marekani, baada ya kile walichosema ni uchokozi wa waziwazi wa Washington.
Kwenye hotuba yake kupitia televisheni mara tu baada ya mashambulizi ya Marekani, kiongozi wao, Abdelmalik Al-Houthi alisema Yemen itajibu pigo kwa pigo.
"Huu ndio muelekeo wetu. Jana, majeshi yetu yalifanya mashambulizi ya makombora na droni hapo hapo kujibu mashambulizi ya Marekani dhidi ya nchi yetu. Hivyo huu ni uamuzi wetu, ni chaguo letu, ni muelekeo wetu. Kadiri adui wa Kimarekani anavyoendelea na uchokozi dhidi ya nchi yetu, meli zake za kijeshi zitaendelea kuwa shabaha za droni na makombora." Alisema kiongozi huyo.
Soma zaidi: Wahuthi wa Yemen wanuia kuanza tena kuzishambulia meli za Israel
Al-Houthi alisisitiza kuwa uamuzi wa kuziwekea vikwazo meli zenye mafungamano na Israel sasa unajumuisha pia meli zote za Marekani, akizituhumu nchi hizo mbili kwa kuendeleza uchokozi wake unaoziathiri safari za baharini pale zinapoigeuza bahari kuwa "uwanja wa kivita."
Mashambulizi dhidi ya USS Harry S. Truman
Msemaji wa kijeshi wa kundi la Ansarullah, Yahya Saree, alisema kwamba jeshi limeishambulia meli ya kijeshi ya Marekani, USS Harry S. Truman, kwa makombora na droni alfajiri ya Jumatatu (Machi 17) kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani.
Marekani kwa upande wake ilisema makombora na droni zote za kundi hilo kuelekea meli hiyo zilidunguliwa kabla ya kuleta madhara.
Soma zaidi: Kuongezeka ukandamizaji Yemen kunazorotesha misaada ya kiutu
Kundi la Ansarullah lilikuwa limesitisha mashambulizi yake dhidi ya meli zinazopita kwenye Bahari ya Shamu, mara tu baada ya makubaliano ya usitishaji mapigano kuanza kutekelezwa baina ya Israel na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, lakini wiki iliyopita lilitangaza kurejea tena kwenye kampeni yake hiyo baada ya Israel kuzuwia ufikishwaji wa misaada ya kiutu kwa watu wa Gaza.
Marekani na Israel zinaituhumu Iran kuhusika na operesheni zinazofanywa na kundi la Ansarullah, tuhuma ambazo Tehran imekuwa ikizikanusha.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito wa pande zote kujiepusha na kuuendeleza mzozo huo, huku akionya juu ya kitisho kikubwa cha kuifanya hali ya kibinaadamu nchini Yemen kuzidi kuwa mbaya.