Mataifa ya magharibi yawataka raia wake kuondoka Goma
25 Januari 2025Hayo ni kutokana na mapambano makali yanayoendelea nje kidogo ya mji wa Goma, kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wapiganaji wa kundi la M23. Kupitia taarifa zilizotumwa kwa njia mbalimbali za mawasiliano, raia wa Marekani, Uingereza na Ufaransa wamehimizwa kuondoka haraka iwezekanavyo katika mji wa Goma wakati huu viwanja vya ndege na mipaka ikiwa bado iko wazi.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO , umesema vikosi vyake vya kulinda amani, vinashiriki katika mapigano makali na kwamba vimeshambulia ngome za M23. Jana, serikali ya Kongo ilithibitisha taarifa ya kuuawa kwa kwa gavana wa kijeshi wa jimbo la Kivu Kaskazini, Jenerali Peter Chirimwami.
Haya yanajiri huku duru za kidiplomasia zikisema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana siku ya Jumatatu kujadili ghasia zinazoendelea mashariki mwa Kongo.