Marekani na Urusi zakubaliana kumaliza vita Ukraine
19 Februari 2025Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na Urusi walikutana kwa takriban masaa manne katika kasri la Diriyah mjini Riyadh, Saudi Arabia, na wameafikiana kuanzisha juhudi za kuvimaliza vita vya Ukraine kwa kuunda timu ya wapatanishi, lakini wakakubaliana pia kurekebisha mahusiano yao ya kidiplomasia na kiuchumi, katika kile kinachotazamiwa kama mabadiliko makubwa ya kisera kati ya Washington na Moscow tangu Urusi ilipoivamia Ukraine karibu miaka mitatu iliyopita.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov ambao kwa pamoja wamesema majadiliano hayo ya Riyadh yalikuwa na manufaa makubwa na kuwa ni hatua nzuri ya kwanza.
Soma pia: Urusi na Marekani zakubaliana kufanya mazungumzo bila ya Ukraine
Wengine waliohudhuria mazungumzo hayo ya ngazi ya juu ni mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, Michael Waltz, na mjumbe maalum wa Mashariki ya Kati, Steven Witkoff, huku Urusi ikiwakilishwa pia na mshauri wa mambo ya nje wa Rais Vladimir Putin, Yuri Ushakov.
Hata hivyo, hakuna afisa yeyote wa Ukraine wala wa nchi washirika wa Ulaya aliyeshiriki mazungumzo hayo, jambo lililoibua wasiwasi mkubwa kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ambaye alitangaza kuwa nchi yake haitakubali matokeo yoyote ya mazungumzo hayo. Zelensky aliahirisha pia ziara yake iliyopangwa kufanyika nchini Saudi Arabia hadi mwezi ujao, akisema hakutaka ihusishwe na mazungumzo ambayo nchi yake haikualikwa.
Ukraine na mataifa ya Ulaya hayakushiriki mazungumzo ya Riyadh
Katika mkutano wa Jumatatu usiku mjini Paris, Ufaransa, wa viongozi 11 wa nchi za Ulaya walitahadharisha kuwa hakuna mchakato utakaofanisha amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine ikiwa nchi iliyoshambuliwa na washirika wake wa Ulaya hawatoshirikishwa.
Mara baada ya mazungumzo ya Riyadh kukamilika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alizungumza na wenzake wa Ulaya ili kuwaeleza kilichojadiliwa na mambo yaliyofikiwa. Rubio alizungumza na mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Russia, USA, zakubaliana kufikisha mwisho vita Ukraine
Mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas alimwambia Rubio usiku wa jana jumanne kuwa Marekani haipaswi kunasa katika "mitego" iliyowekwa na Urusi hasa kwa kujaribu kuzigawanya nchi za Magharibi, akisisitiza kuwa Ulaya kwa kushirikiana na Marekani, zinaweza kufikia amani ya haki na ya kudumu kwa kuzingatia masharti ya Ukraine.
"Mazungumzo yanafanyika kwa kuzingatia masharti ya Urusi"
Wachambuzi wanasema mazungumzo haya ya Riyadh ni kama ushindi kwa Urusi na pigo kwa mataifa ya Ulaya kwa kuwa Washington imeingia kwenye mazungumzo kwa kufuata masharti ya Moscow. Wazo ambalo linaungwa pia mkono na Nigel Gould-Davies, mtaalamu wa masuala ya Urusi, Asia na Ulaya katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati:
"Tangu mwanzoni, mazungumzo haya yanaonekana kuegemea upande wa Urusi. Na swali ni ikiwa yanapaswa kuitwa mazungumzo au kwa kiasi fulani, kusalimu amri kwa Marekani. Rais Vladimir Putin anajadiliana huku akilenga ni kwa kiasi gani anaweza kuivuta Marekani ili ikukubaliane na masharti yake ili kufikiwe usitishwaji wa mapigano au kukomesha kabisa vita hivyo. Lakini yote haya kwa masharti ya Urusi. Putin amekuwa wazi kwamba anataka tu kujadiliana na Marekani kuhusu usalama jumla wa Ulaya. Na tayari amefanikisha hilo. Kimsingi, majadiliano haya yanafanyika chini ya masharti ya Urusi na Marekani haikujaribu hata kulipinga hilo."
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amepinga mitazamo hiyo kwa kusema kuwa ili kuumaliza mzozo huo inategemea na utayari wa kila upande kukubaliana na mambo fulani:
" ili kumaliza mzozo wa aina yoyote, lazima kuwe na makubaliano ya pande zote. Hatuwezi kuamua masharti ya upande wa pili. Hatuwezi pia kulijadili hilo leo au katika mkutano na waandishi wa habari. Umoja wa Ulaya utalazimika kushirikishwa mezani wakati fulani, kwa sababu kuna vikwazo pia walivyoweikea Urusi."
Hata hivyo, Urusi na Marekani zimesema mazungumzo hayo ya Riyadh ni mwanzo tu wa mazungumzo marefu yanayohitaji kazi kubwa ya ziada, na kwamba ikiwa yatafanikiwa kumaliza vita vya Ukraine, yanaweza kufungua milango kwa ushirikiano mpana wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
(Vyanzo: AFP, DPA, Reuters, AP)
DW Kiswahili Habari za Ulimwengu | Februari 18, 2025 | Jioni | Swahili Habari leo | Podcast