US, Urusi waafikiana kuanzisha mchakato wa amani Ukraine
19 Februari 2025Trump amesema sasa ana imani kuwa atakutana na rais wa Urusi Vladimir Putin kabla ya mwezi huu kumalizika.
Hayo ni baada ya kukamilika kwa mazungumzo ya mjini Riyadh-Saudi Arabia ambapo viongozi wa ngazi za juu wa Urusi na Marekani walikubaliana kuanzisha timu ya wapatishi ili kuanzisha rasmi mchakato wa amani.
Hata hivyo Urusi imetilia mkazo masharti yake kwa jumuiya ya kujihami ya NATO, kufuta ahadi yake ya mwaka 2008 ya kuipatia Ukraine uanachama, na kupinga kuwekwa kwa vikosi vya muungano huo wa kijeshi nchini Ukraine.
Soma pia:Urusi na Marekani zakubaliana kufanya mazungumzo bila ya Ukraine
Viongozi wa Ukraine na Ulaya hawakushiriki mazungumzo hayo ya Riyadh, lakini waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio alizungumza na wenzake wa Ulaya baada ya mkutano huo, na kusisitiza kuwa Ulaya itashirikishwa wakati muafaka kwa kuwa ina nafasi muhimu katika mazungumzo hayo.