Marekani, EU zaendeleza juhudi za kuutatua mzozo wa Ukraine
27 Februari 2025Kwa upande mmoja, Marekani na Urusi zinaendelea na harakati za kusaka amani huku mataifa ya Ulaya kwa upande mwingine yakifanya kila liwezekanalo ili kutotengwa katika mchakato huo.
Tukianza kwa kuangazia suala la mapigano, Urusi na Ukraine zilishambuliana kwa makombora na droni usiku wa kuamkia leo ambapo wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema ilifanikiwa kudungua droni 19 katika eneo ililolinyakua kinyume cha sheria la rasi ya Crimea, huku mtu mmoja akiripotiwa kuuawa katika mkoa wa mpakani wa Belgorod wa Urusi.
Moscow ilifanya pia mashambulizi kadhaa nchini Ukraine, Mkuu wa jeshi Kyiv Oleksandr Syrskyi, amesema vikosi vya nchi hiyo vimeungana ili kuulinda mji wa Novopavlivka mkoani Donetsk ambako mashambulizi ya Urusi yameripotiwa kuongezeka.
Soma pia: Macron awaambia wenzake wa EU alichozungumza na Trump
Hayo yakiarifiwa, juhudi zinaendelea ili kujaribu kuumaliza mzozo huo. Maafisa wakuu wa Marekani na Urusi wanakutana leo mjini Istanbul Uturuki ili kujadiliana namna ya kurekebisha mahusiano yao ya kutatua masuala ya kidiplomasia. Ikumbukwe kuwa Uturuki ambayo pia ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO ilijaribu mara mbili mnamo mwaka 2022 kuchukua jukumu la kusimamia mazungumzo ya kumaliza uhasama nchini Ukraine.
Hatua hii inakuja baada ya mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na yule wa Marekani Marco Rubio yaliyofanyika Februari 18 katika mji mkuu wa Saudia- Riyadh, ambapo walianzisha mazungumzo kuhusu mzozo wa Ukraine, bila kuihusisha Kyiv wala washirika wa Ulaya.
Harakati za mataifa ya Ulaya kujaribu kubadili msimamo wa Marekani
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer yuko mjini Washington ambako leo hii anatarajia kuzungumza na rais Donald Trump ili kujaribu kupata hakikisho kuwa Marekani itatoa dhamana ya usalama ili kuizuia Urusi kuivamia tena Ukraine baada ya makubaliano yoyote ya amani, jambo ambalo Trump ameonyesha kulipinga mara kadhaa akisema kuwa Ulaya ndio yenye jukumu la kuilinda Ukraine.
"Sitotoa dhamana ya usalama zaidi. Tunataraji Ulaya ifanye hivyo kwa sababu hapa tunamzungumzia jirani yao wa karibu, lakini tutahakikisha kila kitu kinakwenda sawa."
Aidha, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amealikwa kuhudhuria mkutano maalum wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika mjini Brussels-Ubelgiji wiki ijayo, mkutano wa kilele utakaojadili uungwaji mkono na dhamana ya ulinzi kwa Ukraine.
Katika barua rasmi ya mualiko iliyochapishwa leo Alhamisi, Rais wa Baraza la Ulaya António Costa alimueleza Zelenskiy kuwa kwa sasa kuna ari mpya ambayo inaweza kusababisha amani jumla, ya haki na ya kudumu. Mkutano huo wa Machi 6 umeitishwa ili kujadili namna ya kujibu mabadiliko makubwa ya sera ya Marekani kuhusu vita vya Ukraine.
(Vyanzo: Mashirika)