Marekani na Ukraine zazungumzia kuhusu madini ya Kyiv
21 Februari 2025Ukraine na Marekani zinafanya mazungumzo ya makubaliano ya kuipatia Marekani fursa ya kufikia hifadhi ya madini ya Ukraine, licha ya mzozo mkubwa kati ya rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky na mwenzake wa Marekani Donald Trump.
Chanzo kimoja nchini Ukraine kimeliarifu shirika la habari la AFP hii leo. Afisa mmoja mkuu wa Ukraine mwenye ufahamu kuhusu suala hilo, ameiambia AFP kwamba licha ya mvutano kati ya Zelensky na Trump, mazungumzo juu ya uwezekano wa makubaliano hayo yanaendelea leo. Soma: Ukraine: Trump 'yuko katika ulimwengu wa upotoshaji', asema Zelensky
Ukraine ilikuwa imekataa jaribio la kwanza la timu ya Trump la kuingia katika makubaliano kuhusu raslimali asili za Ukraine
na kusema pendekezo hilo halijumuishi dhamana za usalama kwa Ukraine, hatua iliyomkasirisha Trump.
Chanzo hicho cha Ukraine kimesema kuna ubadilishanaji wa mara kwa mara wa rasimu za makubaliano na kuongeza kuwa walituma nyingine jana na kwamba Ukraine sasa inasubiri majibu ya Marekani.