Marekani na Korea Kaskazini zatunishiana misuli ya kijeshi
2 Machi 2025Meli iliyobeba ndege za kijeshi za Marekani imewasili leo Jumapili nchini Korea Kusini siku chache baada ya Korea Kaskazini kuzinduwa makombora yake chapa Cruise yaliyokuwa yanaonesha uwezo wake wa kufanya mashambulizi.
Meli hiyo ya Carl Vinson iliyobeba ndege hizo na vifaa vya kijeshi imewasili katika bandari ya Busan ikiwa ni kuonesha uimara wa ushirikiano mkubwa wa kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini katika wakati ambapo kuna vitisho vya kijeshi vinavoendelea kutolewa na Korea Kaskazini.
Soma zaidi. Israel yasimamisha usafirishaji wa misaada kuingiza Gaza
Tangu kuapishwa Januari 20, Rais wa Marekani Donald Trump alisema atawasiliana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ili kufufua mazungumzo ya kidiplomasia lakini Korea Kaskazini haijajibu ombi hilo la Trump na inaelezwa kwamba uhasama unaodaiwa kuongozwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini umezidi tangu kuapishwa kwa Trump.
Wataalamu wanasema kuna uwezekano kwamba Kim Jong Un hatokubali ombi hilo la Trump kwa kuwa kwa sasa anaangazia zaidi uungaji mkono wake kwa Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.