Marekani na Iran kujadili mpango wa nyuklia
11 Aprili 2025Msemaji wa sera za kigeni wa umoja huo, Anouar El Anouni, alisema wanazingatia mazungumzo yaliyotangazwa kati ya Marekani na Iran na kuongeza kuwa hatua zozote kuelekea kuongeza fursa za matokeo ya kidiplomasia ni za mwelekeo bora.
Wakati huo huo,Iran ilisema inaipa diplomasia fursa halisi na ya kweli katika mazungumzo ya nyuklia na Marekani licha ya shinikizo linalozidi kutoka kwa serikali ya mjini Washington, kuweka mazingira ya malumbano nchini Oman mwishoni mwa wiki hii.
Mahasimu wa muda mrefu Iran na Marekani wanajiandaa kufanya mazungumzo mjini Muscat siku ya Jumamosi yanayolenga kufikia mkataba wa nyuklia.
Jumatatu wiki hii Rais wa Marekani Donald Trump alitoa tangazo la kushangaza kwamba utawala wake utafungua mazungumzo na Iran.
Mshauri wa cheo cha juu wa kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema Ijumaa kabla mazungumzo ya Oman kwamba Iran inataka mkataba halisi wa haki na Marekani.