Marekani kupeleka 'silaha zaidi' Ukraine: Trump
8 Julai 2025Tangazo la Trump linajiri baada ya Washington kusema wiki iliyopita kuwa inasitisha baadhi ya shehena za silaha Kwenda Kyiv, na kuwaacha maafisa wa Ukraine wakihangaika kutafuta ufafanuzi.
Soma pia: Trump: Marekani kuitumia silaha zaidi Ukraine
Kusitishwa upelekaji silaha kunaweza kuleta changamoto kubwa kwa Kyiv, ambayo inakabiliana na mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi katika vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Lakini akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Trump alisema: "Tutapeleka silaha nyingine zaidi. Inabidi tufanye hivyo. Wanapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda. Sasa hivi wanashambuliwa sana. Wanapigwa sana. Itabidi tupeleke silaha zaidi. Ndio, kimsingi ni silaha za kujihami. Lakini wanapigwa sana sana."
Ahadi ya rais huyo wa Marekani ya kupeleka zana zaidi za kivita nchini Ukraine inajiri baada ya Moscow kusema jana kuwa askari wake walikikamata Kijiji chake cha kwanza katika mkoa wa kati wa Dnipropetrovsk nchini Ukraine baada ya kuelekea huko kwa miezi kadhaa.
Urusi ilianzisha mashambulizi mapya ya ndege zisizo na rubani na makombora kabla ya tangazo hilo, ikiwa ni pamoja na vituo vya kuandikisha wanajeshi wa Ukraine.
Soma pia: Mashambulizi kati ya Urusi na Ukraine yasababisha kusitishwa safari za ndege
Kyiv pia ilisema ilifanya shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye kiwanda cha silaha cha Urusi katika mkoa wa Moscow.
Urusi ilisema kuwa vikosi vyake viliteka kijiji cha Dachne katika eneo la Dnipropetrovsk, eneo muhimu la uchimbaji madini ambalo limekuwa chini ya mashambulizi ya anga ya Urusi. Kyiv mpaka sasa inakanusha kuwepo kwa mafanikio yoyote ya Urusi kwenye mkoa wa Dnipropetrovsk.
Trump alionyesha kusikitishwa kwake na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Rais huyo wa Marekani ametatizika kupata suluhu ya vita nchini Ukraine lakini anashikilia kuwa amedhamiria kuuhitimisha haraka mzozo huo ambao alikuwa ameahidi wakati wa kampeni za uchaguzi kumaliza katika siku ya Kwanza ya muhula wake wa pili.
Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekubali kumuondoa balozi wa Ukraine nchini Marekani, Oksana Markarova. Hayo yalikubaliwa katika mazungumzo ya simu kati ya Zelensky na Trump.
Pande zote mbili sasa zinafanya mazungumzo ya kumtafuta mrithi wake, ambaye atahitaji idhini kutoka kwa nchi zote mbili. Markarova, ambaye amehudumu kama balozi wa Washington tangu 2021, amekosolewa na baadhi ya Warepublican kwa kuegemea zaidi chama cha Democratic.
afp, ap