Marekani kuipatia Ukraine mifumo ya ulinzi ya Patriot
14 Julai 2025Kiongozi huyo wa Marekani ametangaza uamuzi huo alipozungumza na waandishi habari wakati akirejea Washington baada ya kuhudhuria mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu iliyofanyika huko New Jersey.
Trump ametangaza hatua hiyo katika wakati anaonesha kufadhaishwa na kushindwa kwa juhudi zake za kumshawishi Rais Vladimir Putin wa Urusi avimalize vita vya Ukraine.
Amesema atatoa maelezo ya kutosha baadae hii leo Jumatatu lakini ameashiria kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na mashambulizi ya Urusi yanayoendelea kuilenga Ukraine.
Amesema mifumo hiyo ya Patriot inahitajika sana na Ukraine na gharama zake zitalipiwa na Umoja wa Ulaya.
"Hatutalipa chochote, lakini tutawapelekea, itakuwa biashara kwa upande wetu, kwa hivyo tutawapatia mifumo hii ya Patriot wanayoihitaji sana, kwa sababu (Rais wa Urusi Vladimir) Putin amewashangaza wengi. Anaongea mambo mazuri, halafu baadae usiku anavurumisha mabomu. Kwa hivyo kuna tatizo kidogo hapo. na sipendi hali hiyo", amesema Trump.
Trump hakutaja idadi ya mifumo itakayopelekwa Ukraine lakini amedokeza pia kuwa utawala wake unapanga kuipatia serikali mjini Kyiv silaha zaidi za kisasa kwa ajili ya vita.
Trump kukutana na Katibu Mkuu wa NATO mjini Washington
Baadae wiki hii Rais Trump atakutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami, NATO, Mark Rutte, kwa mazungumzo yatakayogusia pia suala la msaada zaidi wa kijeshi wa Ukraine.
Mtendaji huyo mkuu wa NATO anatazamiwa kuwasili mjini Washington leo Jumatatu. Tangazo la kutumwa mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot limetolewa wakati Washington inaendeleza juhudi za kidiplomasia za kuutanzua mzozo wa Ukraine.
Mjumbe maalumu wa Washington kwa Ukraine Keith Kellogg anaanza hii leo ziara ya wiki nzima nchini Ukraine.
Katika wiki za karibuni Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine ameongeza miito kwa washirika wake wa magharibi kuipatia nchi yake uwezo zaidi wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora na droni kutoka Urusi.
Trump ambaye aliingia madarakani akiahidi kuvimaliza vita vya Ukraine ndani ya muda mfupi, amesema mara kadhaa kuwa amevunwa moyo na tabia isiyotabirika inayooneshwa na Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Trump afadhaishwa na kutotabirika kwa Rais Putin
Licha ya mazungumzo kadhaa kwa njia ya simu kati ya Trump na Putin pamoja na Trump kuzuia nyongeza ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Moscow, kiongozi huyo wa Urusi hajaonesha dhamira ya kulegeza kamba na badala yake amezidisha mashambulizi ndani ya Ukraine.
Kutokana na mafanikio haba ya juhudi zake za kumuenga enga kiongozi huyo wa Urusi, rais Trump ameashiria hapo jana kuwa huenda atachukua hatua za kuongeza mbinyo dhidi ya Moscow.
Bunge la Marekani lilipitisha jana Jumapili muswada unaompa Trump uwanja mpana wa kuchagua iwapo atalenga kuiwekea Urusi vikwazo vikali vya kiuchumi.
Seneta wa chama cha Republican, Lindsey Graham, amesema muswada huo unamruhusu Trump "kuulenga uchumi wa Urusi, na nchi zote zinazimsaidia Putin kuendelea na vita".