Marekani kuikabidhi Iraq serikali ya mpito mwakani
16 Novemba 2003BAGHDAD: Tayari hapo mwezi wa Juni mwakani, Marekani ina niya ya kuikabidhi serikali mpya ya mpito ya Iraq jukumu la kisiasa. Taarifa hiyo ilitolewa na Jalal Talabani, Rais wa Baraza Tawala la Iraq lililoteuliwa na Marekani, baada ya mazungumzo yaliyofanyika kati ya Baraza hilo la Mtawala wa Kimarekani, Paul Bremer. Huo utakuwa pia mwisho wa kukaliwa rasmi Iraq na wanajeshi wa kigeni, alisema Bwana Talabani. Hata hivyo alisisitiza kuwa wanajeshi hao wa mwungano hawatoihama Iraq hapo hapo, bali watakabidhiwa jukumu jipya. Kwa mujibu wa mpango huo mpya hapo mwanzoni mwa mwaka ujao 2004 viongozi wa makabila kutoka mikoa 18 ya Kiiraq watawachagua wawakilishi wao pamoja na viongozi wengine wa kisiasa katika Bunge jipya la Taifa. Bunge hilo litaichagua serikali mpya ya mpito itakayokabidhiwa madaraka yake na mtawala wa Kimarekani. Nayo serikali hiyo mpya ya mpito itapaswa kutunga katiba mpya itakayowaita raiya wa Iraq walichague bunge rasmi hadi mwishoni mwa mwaka 2005.